Care International /WWF Yatoa Vitendea Kazi kwa Waganikazi Wasaidizi
Hafla hii imefanyika Februari 14, 2023 na Shirika la Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori (Wild Wide Fund for Nature - WWF) na Care International inayotekeleza Mradi wa Miaka Mitatu kwa Vikundi vya Hisa kwa Usalama wa Chakula na Uendelezaji Mazingira, kupitia CARE – WWF Alliance, katika vijiji tisa vya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Akitoa hotuba yake katika Hafla hiyo ya kukabidhi vifaa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Stephen Mhapa amesema, “Nawashukuru CARE-WWF Alliance kwa kazi hii ambayo ilitakiwa ifanywe na Serikali, asante sana kwa ushirikiano huu”.
“Katika maendeleo ni lazima aanze mtu mmoja, inafuata Kaya kisha vikundi mbalimbali. Vikundi vikipata mafunzo ni rahisi kuelimisha wengine ili kuleta mafanikio ya pamoja, hivyo nawasihi vikundi vilivyopata mafunzo haya myatumie kwa tija, ili watu wengine wajifunze kutoka kwenu”. Amesema Mheshimiwa Mhapa.
Mheshimiwa Mhapa amesisitiza kusema kuwa, “Waganikazi wanafanya kazi kama Wataalam wa Kilimo. Mbali na kupewa elimu au mafunzo pia mmepatiwa vitendea kazi ili viweze kurahisha majukumu yenu kwa ufanisi zaidi. Mnatakiwa kujivunia na kujitangaza ili ulimwengu ujue kuwa mnaweza na kuaminiwa”.
Mheshimiwa Mhapa pia amewasihi Waganikazi hao kutunza vifaa walivyopewa ili vidumu muda mrefu na kueleza kuwa, vikundi vishikamane, vifanye vikao kujadili mafanikio na maendeleo ya vikundi vyao, kuwa waaminifu na kupendana.
Mheshimiwa Mhapa pia ameowamba wanavikundi kupanda miti rafiki wa vyanzo vya maji, miti ya matunda na ya kibiashara hasa ya mbao ili kuwaingizia kipato.
Akisoma ripoti ya utekelezaji wa Mradi huo Dkt. Abubakari Kijoji ambaye ni Mratibu wa Mradi amesema, kiasi cha Dola za Kimerekani Milioni 1.5 sawa na fedha za Kitanzania shilingi Bilioni 3.4 zinatekeleza mradi huu ambao unafadhiliwa na Mdau wa Maendeleo toka Uswisi kupitia WWF USA.
Ameongeza kusema kuwa, malengo ya mradi huu ni kuimarisha usalama wa chakula na kipato cha kaya na kuimarisha huduma za Mifumo ya Ikolojia ya Mto Ruaha Mkuu, na kupunguza athari za mazingira zinazotokana na kilimo kisichokuwa endelevu, na kupunguza uharibifu wa misitu na vyanzo vya maji.
Akitaja mafanikio ya mradi kwa kipindi cha miezi 18 Dkt. Kijoji amesema, mradi umeweza kulinda na kuhifadhi rasilimali ardhi, misitu na maji, kutoa hati za ardhi za kimila, kusimamia vyanzo vya maji kwa kupanda miti rafiki na maji, kuandaa vitalu vya miche, kuboresha kilimo, kutoa elimu ya kilimo bora na vikundi kupata mikopo bila riba kutoka Halmashauri.
Dkt. Kijoji pia ametoa ombi kwa Halmashauri kutoa usimamizi wa mipango ya matumizi bora ya ardhi za vijijiji, uungwaji mkono kwa Waheshimiwa Madiwani kwenye kusimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi kama ilivyoidhinishwa katika mpango, wawekezaji, watumia maji na wote wanaonufaika na huduma za ikolojia zinazotokana na uhifadhi ya uendelezwaji wa misitu na vyanzo vya maji wawaunge mkono wananchi, na waganikazi waingizwe kwenye mfumo wa Halmashauri kama nguzo ya muhimu ya kuwafikia wananchi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ambaye ni Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Bi. Lucy Nyallu alikuwa na haya ya kusema, “kupitia mafunzo haya na mashamba darasa, vimesaidia sana kwa jamii kupata elimu, na kwamba Serikali inafanya kazi kwa usaidizi yaani Private Public Partnership (PPP) ili kuweza kufanikiwa vizuri”.
Ameongeza kusema kuwa, wakulima wakizalisha kwa tija, wanaweza kuinua uchumi, kuongeza uzalishaji, pia vijana hawataweza tena Kwenda mijini, kwani fursa zipo huko kwenye maeneo yao.
Bi. Nyallu amewashukuru Wadau kwa kujitoa, na kwamba kama wanahitaji kuongeza vijiji bado vipo vingi kwa ajili ya kujifunza.
Aidha Mkurugenzi wa Shirika la Care International Bi. Haika Mtui ametoa neno lake kwa kusema, anaishukuru Serikali kwa kuwahudumia wananchi kwa kuwapa mikopo isiyo na riba, kwa masuala ya mazingira na kilimo ili kujenga Taifa lenye afya.
Bi. Mtui ameongeza kusema kuwa, kuna upungufu mkubwa sana wa Maafisa Kilimo, lakini kwa kushirikiana na WWF wanajitahidi kutoa elimu kwa wananchi wanaowazunguka kwa kuwatengeneza Waganikazi, ili angalau elimu hii iwafikie wale wachache walio karibu. Pia ameomba watunze vifaa hivyo kwa kufanyia kazi iliyokusudiwa kama urahisi wa kuleta ripoti na kufanya ufuatiliaji kwa wakulima wadogo au vikundi mbalimbali. Mwisho ameomba Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji itoe ushirikiano kwa Waganikazi hawa pale wanapoenda kutoa huduma kwa wananchi.
Mradi huu unatekelezwa katika Kata ya Ifundi kwa vijiji vya Mibikimitali na Udumuka, Kata ya Mgama ni vijiji vya Ibumila na Ilandutwa, Kata ya Lumuli ni vijiji vya Lumuli na Itengulinyi, Kata ya Wasa ni vijiji vya Ufyambe, Mahanzi na Wasa. Mradi huu ulianza kutekelezwa mwezi Juni 2021, ambapo ni mradi wa awamu ya Kwanza uliotekelezwa pia Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa