Atoa maagizo utatuzi wa changamoto ya Wanyama wakali Bwawa la Mtera
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Kheri James amefanya mkutano mkubwa wa kihistoria katika Kijiji cha Migoli Tarafa ya Ismani mapema Agosti 20, 2025 ambapo amezungumza na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kuhusu masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwa ni Pamoja na kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero za wananchi.
Suala kubwa linalowasumbua wananchi katika maeneo ya Tarafa ya Ismani ni Wanyama wakali hususani mamba na viboko kwenye bwawa la mtera Pamoja na tembo kwenye maeneo mengine ya mashamba. Kuhusu mamba na viboko Mhe. Kheri James ametoa maagizo kwa TAWA kwa kushirikiana na maafisa wanyamapori(w) kuhakikisha changamoto hiyo inatafutiwa majawabu.
Wanyama wengine waharibifu kama tembo, Mhe. Kheri James amewaasa wananchi kuchukua tahadhari lakini pia kuzingatia aina ya mazao ya kulima ambayo siyo kivutio cha Wanyama hao.
Aidha Mhe. Kheri James ameweka msisitizo juu ya utunzaji wa bwawa la Mtera kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo na hivyo kuepuka kufanya shughuli za kiuchumi pembezoni mwa bwawa la mtera ikiwemo kilimo na matumizi ya madawa ili kulinda bwawa.
“Bwawa la Mtera ni urithi wa Taifa letu, si mali ya wana Iringa pekee, hivyo ni jukumu la kila mmoja kulitunza na kuepuka shughuli zinazoathiri ikolojia yake ikiwemo uchafuzi wa mazingira” amesema.
Kwenye suala la elimu Mhe. Kheri James amesema serikali inatumia fedha nyingi sana katika ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya elimu na kutoa wito kuwa miundombinu hiyo itumike ipasavyo.
“Mtoto akipata elimu Dunia itamtafuta, yeye hataitafuta Dunia bali Dunia itamtafuta. Somesheni Watoto ukisomesha mtoto elimu ndio kitu pekee kinachomfanya mtu yeyote akawa kitu chochote, mbele ya elimu asiyetakiwa hutakiwa, asiyetafutwa hutafutwa kwa sababu elimu humfanya mtu bora na muhimu anayehitajika katika mazingira yake” Amesema Mhe. Kheri James.
Kwa uopande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Benjamin Sitta ameeleza maendeleo makubwa yaliyokwisha kufanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ikiwa ni kwenye mtandao wa Barabara, maji, elimu na mikopo kwa vijana, watu wenye ulemavu na akinamama.
“Iringa Imara Tutaijenga kwa Umoja na Uwajibikaji”
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa