CMT Iringa DC Yampongeza Mhe. Moyo kwa Utumishi wake
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa ambae kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Nachwingea Mhe. Mohammed Moyo amekutana na kupeana salamu za mwisho na Mkurugenzi Mtendaji, Wakuu wa Idara na Vitengo Halmashauri ya Wilaya Iringa (CMT).
Katika kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji - Kalenga Wakuu wa Idara na Vitengo wamepata nafasi ya kumshukuru Mhe. Moyo kwa kipindi chote alichohudumu kama Muwakilishi wa Rais katika Wilaya ya Iringa, kumshukuru na kumpongeza kwa uchapakazi wake, ustaarabu na namna alivyotumia njia shirikishi katika uongozi wake.
Akizungumza katika kikao hiko kifupi Mkurugenzi Mtendaji Wakili Muhoja amesema anamshukuru na kumpongeza Mhe. Moyo kwani alikuwa akiwapa nafasi na kuwasikiliza Wataalamu wanasema nini na amekuwa akikubali kushauriwa na Wataalamu.
“kiukweli hata kwenye Halmashauri nyingine huko MaDC na MaDED hawasikilizani lakini kwako imekuwa tofauti, tulipata DC ambaye ni muelewa kama wewe kazi ilikuwa na amani”.
Umefanya mengi sana pia katika miradi nakumbuka hata kipindi cha madarasa 94 ziara zile ambazo tulipangiana napita huku, Mwenyekiti anapita kule na wewe unapita kule kwa kweli ilitusaidia sana na hiyo ilikuwa timu ya ushindi ambayo kila mtu angetamani kuwa nayo. Ameongeza.
Aidha amesema Mhe. Moyo amekuwa kiongozi mwema ambaye aliunganisha Chama, Serikali kwa maana ya Halmashauri na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, pia ameahidi yale yote aliyoyaanzisha basi yataendelezwa na Mkuu wa Wilaya Mpya.
Naye Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Bibi Lucy Nyalu amesema Mhe. Moyo amekuwa mchapakazi ameweza kufika katika vijiji vyote na amekuwa mtu wa kuomba ushauri kabla ya kuchukua maamuzi na pia amemuomba kama kuna sehemu ambayo walikwazana basi Mhe. Moyo awasamehe.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Ardhi Ndugu Geofrey Kalua amesema yale yote mema na mazuri aliyoyaacha Mhe. Moyo basi yataendelezwa.
Akizipokea salamu, shukrani na pongezi hizo Mhe. Moyo amewashukuru pia Wakuu wa Idara na Vitengo kwa ushirikiano na amesema kuwa alipochaguliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa alikuwa mgeni sana katika masuala ya Serikali lakini kufanikiwa kwake hasa katika ziara zake ni kutokana na Wakuu wa Idara kwa sababu walimfunza na kumshauri nini cha kufanya.
“yale mazuri yangu mtayachukua na yale mabaya yangu niachieni mwenyewe niende nayo, lakini kufanikiwa kwangu mpaka Mhe. Rais kuniona niendelee ni kutokana na nyie, mmesababisha nionekane nafaa”.
Ninajua tumefanya kazi vizuri na ndio maaana nikamuomba Bashir angalau tuagane, sisi ni binadamu huenda tulikwazana lakini nyie hakuna mtu alionikwaza ninaondoka kwa furaha kwa sababu mmenifunza mengi. Amesema.
Kadhalika amewaasa pia Wakuu wa Idara kumpatia ushirikiano wa kutosha Mkuu wa Wilaya Mpya na kusaidiana katika miradi mikubwa ya maendeleo kama skimu ya umwagiliaji ya Mkombozi nakadharika.
Mhe. Moyo kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea inayopatikana Mkoani Lindi na kwa sasa Wilaya ya Iringa inaongozwa na Mhe. Veronica Kessy.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa