CRDB Yazindua Wiki ya Huduma Kwa Wateja
Katika kufanikisha wateja wa Benki ya CRDB wanafurahia kupata huduma za uhakika na kwa haraka, Benki hiyo imefanya hafla fupi ya uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja Oktoba 02, 2023 katika Tawi la Iringa Mjini.
Hafla hiyo ikiwa na Kaulimbiu isemayo “Team Service” kwa maana ya “Utoaji wa Huduma wa Pamoja” ikiwa na lengo la kuwaleta wateja kwa pamoja na kuwahudumia kwa haraka, na kutoa nafasi kwa mteja kama anahitaji huduma zaidi, maoni na ushauri.
“Mikopo kwa watumishi na wafanyabiashara imeongezwa muda kutoka miaka saba hadi tisa, ili kumrahisishia mteja aweze kulipa mkopo huo bila usumbufu. Pia huduma za Bima kwa kitu chochote iwe biashara, gari, nyumba tunatoa ili mteja atakapopata majanga katika eneo hilo basi aweze kulipwa kupitia Bima aliyokuwa anakatia”.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Kanda Bi. Chabu Mishwaro alipokuwa anatoa hotuba fupi kwenye halfa hiyo. Bi. Chabu ni Meneja kwa Mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Morogoro.
Bi. Chabu ameongoza kuwa, pamoja na huduma za mikopo na Bima, pia kuna huduma nyingi kama Green Bonds, uwekezaji, mrejesho wa kidigitali (Digital Feedback) na kupata faida mbalimbali. CRDB wameenda mbali zaidi na kuanzisha ATM za kuweka pesa ili kuondoa usumbufu wa mtu kukosa sehemu ya kuweka pesa bila kwenda kwa wakala
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Iringa Ndugu Leonard Masanja ambaye alikuwa Mgeni Rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa katika hafla hiyo, amefurahishwa sana kushiriki katika uzinduzi huo wa Wili ya Huduma kwa Wateja na kuwasihi wananchi kuja kuwekeza katika Benki ya CRDB ili wapate faida mbalimbali.
Aidha Ndugu George Kaundama kwa niaba ya wateja wote wa CRDB, amepongeza jitihada za Benki hiyo na kushauri kuwepo na dawati la kusikiliza hoja na shauri mbalimbali kutoka kwa wateja.
Wakati huo huo, CRDB pia waliweza kuongea na Kamati ya Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa lengo la kuwajulisha watumishi huduma zao mbalimbali wanazotoa, na kushauri akauti za shule au miradi ziweze kufunguliwa katika Benki hiyo.
Baadhi ya Wanakamati ya Menejimenti waliweza kuuliza maswali na kutoa shauri mbalimbali katika utoaji wa huduma zao, ikiwa ni pamoja na kuomba kufungua Tawi la CRDB katika Ofisi Kuu za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa zilizopo Kijiji cha Ihemi Kata ya Mgama.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa