Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Kheri James awahimiza wananchi kupitia kuwa na matumizi bora ya ardhi ili kuepuka migogoro inayotokana na matumizi ya ardhi. Mhe. Kheri ameyasema hayo alipokuwa kwenye ziara kusikiliza wananchi, kuhamasisha maendeleo na kukagua miradi katika kata ya Kihanga, Wasa na Maboga June 04, 2024.
Mhe. Kheri amesema maeneo yote yajulikane kulingana na matumizi yake na kwamba wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa maafisa ardhi ili kuweza kupimiwa maeneo yao ambapo hii itasaidia kuondoa migogoro ikiwemo ya wakulima na wafugaji.
“Maeneo yakipimwa yakamilikishwa maana yake kila shamba litakuwa na mwenyewe na huyo mwenyewe atakuwa na hati ya kimila, akiwa na hati ya kimila hakuna mtu atakayevamia kwenye eneo ambalo limepimwa na kumilikishwa”, amesema Mhe. Kheri.
Aidha Mhe. Kheri amesisitiza kuwa ni muhimu kwa maeneo yenye migogoro inayohatarisha ustawi wa wananchi hasa maeneo ya uzalishaji mali lazima imalizwe na kuwaagiza maafisa ardhi wa Halmashauri kuhakikisha wanafika kwenye maeneo yenye migogoro na kufanya utatuzi hasa kwenye kata ya Kihanga na Kiponzelo.
Kwa upande wao, wananchi wa kata husika kupitia kwa viongozi wao wametoa shukrani na pongezi kwa serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi za Miradi ya elimu, afya na barabara. Sanjari na hayo pia wananchi wametoa kero na changamoto mbalimbali ambazo zimechukuliwa kwa ajili ya utatuzi na zingine kutatuliwa au kutolewa ufafanuzi wa papo kwa papo.
Mkuu wa Wilaya ameanza ziara yenye lengo la kuzifikia kata zote 28 za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ili kuwasikiliza wananchi, kuwahamashisha kwenye shughuli za maendeleo na kukagua miradi inayotekelezwa kwenye maeneo husika.
#Iringa Imara, Tutaijenga kwa Umoja na Uwajibikaji.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa