Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Kheri James amefanya ziara katika Tarafa ya Isimani Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Machi 22, 2024 ambapo amepata fursa ya kuongea na watumishi pamoja na wananchi.
Akizungumza na wananchi wa Isimani Mhe. Kheri Jamesi amesema kuwa lengo la serikali ni kuboresha mazingira ya wananchi kufanyia kazi ili kujiingizia kipato “Tumepokea fedha kwenye afya, maji, barabara, tumepokea fedha nyingi sana kwenye skimu za umwagiliaji, tumepokea fedha katika elimu, na kwa kweli kila mtu anashuhudia maana hakuna kata ambayo haijaguswa na mguso wa maendeleo lakini haya yote ambayo Mhe. Rais anayafanya anayafanya kwa faida ya mimi na wewe” amesema Mhe. Kheri.
Aidha, Mhe. Kheri ametoa pongezi zake kwa kazi kubwa inayofanywa na Halmashauri kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kutambua uwepo wa wataalamu wa idara mbalimbali zikiwemo, kilimo na elimu chini ya Mkurugenzi Mtendaji ndg. Robert Masunya.
Kuhusu suala la lishe na utoaji wa chakula mashuleni, Mhe. Kheri amewaasa viongozi ambao vijiji vyao vina miradi inayoingiza mapato, watenge kiasi cha fedha kwa ajili ya chakula cha wanafunzi shuleni. Pia amewataka viongozi wa vijiji na kata kutumia mbinu rafiki kuwafanya watu waelewe na kuchangia chakula cha wanafunzi shuleni.
Mhe. Kheri pia amepata nafasi ya kuwasikiliza wananchi ambapo ametoa maelekezo kuhusu magari ya kubebea wagonjwa na kusema kuwa hakuna kuchangisha wananchi fedha kwa ajili ya mafuta ya gari ya kubebea wagonjwa wala fedha za kufanyia matengenezo kwani serikali inayahudumia magari hayo.
Kwa upande mwingine Mhe. Kheri ametoa maelekezo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kuweka utaratibu wa vijiji kuwa kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuepuka migogoro mbalimbali ya ardhi ikiwemo migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
Nao wananchi wa tarafa ya Isimani wameishukuru Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea miradi ambayo imekuwa msaada mkubwa sana kwao ikiwemo miradi ya maji.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa