“Natoa Siku Saba Mita za Maji Zilizoibiwa Zirudishwe” – DC Kessy
Wananchi wa Kijiji cha Kiponzero Kata ya Maboga wamepewa siku saba kurudisha mita za maji zilizoibiwa katika mabomba mbalimbali, kufuatia mgogoro uliopo kati ya wananchi na Mwenyekiti wa Kijiji hicho ambapo wananchi hawataki kulipia huduma za maji.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Veronica Kessy alipokwenda kutatua mgogoro kati ya wananchi na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiponzero Ndugu Allen Exavery Dallu siku ya Jumatano tarehe 06/09/2023
“wananchi mnafanya kosa kubwa kuiba mita za maji na kumuondoa Mwenyekiti wa Kijiji madarakani, kwa madai yenu kuwa hamumuhitaji bila sababu za msingi. Inatakiwa mfuate sheria, kanuni na taratibu kwani Mwenyekiti huyo amekuwepo kwa sheria na taratibu. Kuazia sasa natoa siku saba mita za maji zirudishwe na walioiba mita hizo watachukuliwa hatua, pia Mwenyekiti bado yupo madarakani kama kawaida”.
Aidha Mheshimiwa Kessy amesisitiza suala la kulinda mazingira na kutunza vyanzo vya maji kwa kufanya usafi na kupandi miti kwa wingi ambayo ni rafiki wa maji. Pia suala la lishe limkuwa tatizo katika jamii ya Iringa na kuongeza kusema kuwa, ni muhimu kupanda miti ya matunda na kuwapatia watoto mlo kamili ili kuondokana na udumavu.
Naye Mwanasheria wa Halmashauri Bi. Stella Makali aliwasomea wananchi sheria na taratibu zinazopaswa kufuatwa endapo kunakuwa na tatizo kama hilo.
Naye Meneja wa Mamlaka ya Maji Vijijini (RUWASA) Mhandisi Exaud Humbo amesema, “mwananchi anatakiwa kuchangia huduma za maji ili kwamba miundombinu ikiharibika inakuwa rahisi kutumia pesa zilizochangiwa kurekebisha”.
Mhandisi Humbo ameendelea kusema kuwa, “miundombinu ya kijiji hiki ni ya muda mrefu hiyo kutotosheleza mahitaji ya maji kwa wananchi kwa wakati mmoja. Serikali imeleta kiasi cha Shilingi Bilioni 4 kwa ajili ya kujenga upya miundombinu ya maji ambayo itakuwa mkombozi kwa kero za maji. Michoro ipo tayari kilichobaki ni kuanza kazi tu”
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Komredi Costantine Kihwele alikuwa na haya ya kusema “Serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inatoa fedha nyingi kutekeleza miradi mbalimbali kwa ajili ya wananchi wake. Lakini ninyi mnaharibu miundombinu ambayo ipo kwa faida yenu, jambo hili haliwezi kufumbiwa macho. Ninyi wananchi mnatakiwa kuwa wa kwanza katika kulinda rasilimali hizi kwa ajili ya vizazi vyenu.
Wananchi walipata nafasi ya kutoa kero zao mbalimbali, ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara. Mheshimiwa Kessy alichukua kero zao na kuahidi kufanyika kazi hivi punde.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa