DC Moyo Aagiza Elimu Itolewa Kuhusu Chanjo ya Matone ya Ugonjwa wa Polio
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Mohammed Moyo ameitaka Kamati ya Msingi ya Afya ya Jamii kuendelea kutoa elimu kuhusu ugonjwa wa polio kwa wananchi wote na kuwaelezea umuhimu wa chanjo hiyo kupitia majukwaa mbalimbali zikiwemo Taasisi wanazofanyia kazi.
Aidha amewataka kutoa taarifa za utekelezaji wa kampeni katika ngazi mbalimbali ikiwemo kusimamia shughuli zote za kampeni katika eneo au Taasisi zao.
Ameyasema hayo mapema leo Novemba 29, 2022 katika kikao cha Kamati ya Msingi ya Afya ya Jamii kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kikiwa na lengo la kutoa mafunzo kwa kamati hiyo
“Lengo la kampeni hii ni kuwa mabalozi wa kuendesha kampeni dhidi ya ugonjwa huu hatari wa Polio kwa kuhamasisha watoto wote katika jamii zetu walio chini ya miaka mitano wapatiwe chanjo ya Matone ya Polio.”
Aidha nawasisitiza mkaendelee kuihamasisha kampeni hii ili iweze kufanikiwa, Hapa Mwenyekiti wa Halmashauri upo katika majukwaa au vikao vyako huko basi pia utumie fursa hiyo kuhamasisha kampeni hii ya Chanjo ya Matone ya Polio. Ameongeza.
Naye Mkuu wa Idara ya Afya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Dokta Samwel Marwa amewahakikishia kuhusu usalama wa chanjo ya polio kuwa haina madhara yoyote hivyo ni salama kwa watoto na ikiingia mwilini hutoka kwa njia ya haja ndogo, kubwa au kucheua.
“Ninapenda kuwahakikishia tu kuwa chanjo hii inatumiwa na inafanya kazi vizuri zaidi kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na haina changamoto yoyote.” Amesema.
Akitoa ufafanuzi wa chanjo ya polio Mratibu wa Huduma za Chanjo Wilaya Ndugu Sospeter Tiyara amesema polio ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya polio, Ugonjwa huu unapelekea kupooza na hatimaye kifo na amesema ugonjwa wa polio hauna tiba lakini unaweza kuzuiliwa kwa kupata chanjo ya matone ya polio.
“kwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imetekeleza utoaji wa chanjo ya polio ya matone kwa awamu 2, kwa maana ya awamu ya pili na tatu kwa nchi nzima. Awamu ya pili walengwa walikuwa 47,158 waliochanjwa 51646 sawa na asilimia 110% na awamu ya tatu walengwa walikuwa ni 53,191 Waliochanjwa 55,055 sawa na asilimia 103.50”.
Mratibu wa Chanjo Ndugu Tiyara amesema chanjo ya polio ya matone awamu ya tatu itafanyika Tanzania Bara pamoja na Zanzibar na kampeni hiyo itaanza rasmi tarehe 01 hadi 04 Disemba 2022 na wahamasihaji wataanza shughuli za uhamasishaji siku mbili kabla ya kuanza kampeni na kampeni hizi zitafanyika nyumba kwa nyumba na maeneo mengine kuhakikisha watoto wote walengwa wanafikiwa.
Sambamba na uchanjaji huduma zingine ziatatolewa ikiwemo elimu ya chanjo, kuimarisha huduma za chanjo katika vituo vya kutolea chanjo pamoja na kuwatafuta na kuwafatilia watoto wote wenye umri chini ya miaka kumi na tano ambao wamepata ulemavu wa ghafla tepetepe (washukiwa wa ugonjwa wa polio) na kutoa taarifa katika vituo vya karibu kwa uchunguzi na kubaini ugonjwa huu wa polio.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa