DC Moyo Awataka Wananchi wa Iringa Kuachana na Kilimo cha Vinyungu
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Mohammed Moyo amewataka wananchi wa Wilaya ya Iringa kuachana na kilimo cha karibu na vyanzo vya maji maarufu kama kilimo cha vinyungu, kwani sheria imekataza kufanya shughuli zozote za kibinadamu mita sitini kutoka kwenye vyanzo vya maji.
Amesema siasa haihitajiki kwenye uharibifu wa vyanzo vya maji kwani Serikali imeelekeza namna ya kutunza mazingira hivyo amesema lazima kuwepo na ushirikiano kati ya viongozi wa vyama na wananchi katika kutunza mazigira na kukemea watu wanaoharibu vyanzo vya maji na mazingira kiujumla.
Ameyasema hayo mapema leo alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Magubike Kata ya Nzihi katika viunga vya Shule ya Sekondari ya Dimitrios alipokwenda kufanya ufunguzi wa Kampeni ya Upandaji Miti Kiwilaya iliyofanyika mahali hapo.
“Leo ni siku ya uzinduzi wa upandaji miti kiwilaya, hivyo upandaji wa miti ulishaanza na utaendelea mpaka mvua zitakapokaribia kukatika. Hivyo basi kila mwananchi, watu binafsi, vikundi, Taasisi mtatakiwa kushiriki kikamilifu katika kupanda na kuotesha miti katika maeneo yenu kwa kipindi hiki cha mvua”.
Sambamba na kupanda miti mhakikishe kuwa miti mnayoipanda muipande vizuri kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu wetu ikiwa ni pamoja na kupalilia mstari uliopandwa miti ili kuondoa magugu, kuilinda miti dhidi ya mifugo na kuzuia moto kwa kusembua barabara iliyozunguka miti. Ameongeza.
Mhe Moyo amesema ili kutimiza lengo la kitaifa Wilaya ya Iringa imeotesha miti milioni tano laki tatu na thelathini na sita elfu mia tatu na ishirini na nane kwa ajili ya kupanda msimu huu wa mwaka 2022/2023.
“Kama ilivyosomwa kwenye taarifa ya Wilaya ambayo ni asilimia 355.7 ya lengo la Halmashauri, Juhudi zaidi zinahitajika ili kupambana na upungufu wa miti kwa ajili ya matumizi mbalimbali”.
Hivyo DC Moyo amewahimiza wananchi wote kuona na kuitumia fursa hiyo adhimu na kuamua kuanzisha mashamba ya miti ili pamoja na manufaa mengine waweza kujikwamua kiuchumi.
Akisoma taarifa ya upandaji miti wilaya Afisa Misitu Joachimu Mshana amesema Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imeweka malengo ya kupanda miti 1,500,000 kila mwaka na katika msimu huu wa mwaka 2022/2023, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali wameweza kuotesha miche 5,336,328 ya mbao, matunda, kivuli, hivyo kufikia utekelezaji wa lengo kwa asilimia 335.7.
“Mkakati huo umefanikiwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kuongezeka kwa uwekezaji katika upandaji miti kutokana na manufaa mbalimbali wananchi wanayoyapata pamoja na hamasa inayoendelea kutolewa na Serikali pamoja na wadaumbalimbali”.
Ndugu Mshana amesema jumla ya miche ya miti elfu moja (1000) inatarajiwa kupandwa katika maeneo ya Shule ya Sekondari ya Dimitrious, na katika Kata ya Nzihi zaidi ya miche ya miti laki mbili (200,000) ya aina mbalimbali inatarajiwa kupandwa katika maeneo ya mashamba ya watu binafsi na Taasisi mbalimbali.
Aidha Ndugu Mshana amewashukuru wadau mbalimbali wanaojihusisha na upandaji miti katika Halmashauri wakiwa ni pamoja na Mradi wa Urejeshaji endelevu wa mazingira (Sustainable Landscape Restoration SLR), Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF), Taasisi ya Clinton Development Initiative, World Vision, pamoja na waoteshaji wote binafsi katika Halmashauri.
Maadhimisho ya uzinduzi wa upandaji miti kwa mwaka 2022/2023 yana kauli mbiu isemayo “Miti Mazingira Yangu, Tanzania Yangu Naipenda Daima”.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa