Halmashauri Kuu ya CCM Yafurahishwa na Utekelezaji wa Ilani
Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imefurahishwa na utakelezaji mzuri wa Ilani kwa kusimamia miradi mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Mkutano huo umefanyika Septemba 07, 2023, katika Ukumbi wa Halmashauri wa Siasa ni Kilimo.
Akiongea katika hotuba yake fupi katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya Komredi Costantine Kihwele amesema “kuna mtu ametokea CCM na kuna mtu amepitia CCM, hawa ni watu wawili tofauti. Namaanisha kuwa, huyu Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Veronica Kessy ametokea CCM, hivyo nampongeza kwa utekelezaji mzuri wa Ilani katika kusimamia miradi mbalimbali. Amenipa ushirikiano wa kutosha kwa kila jambo, hivyo nampongeza sana”.
Aidha Ndugu Kihwele amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja na Menejimenti yake kwa ujumla kwa usimamizi mzuri na wa uwazi katika kusimamia miradi ya Halmashauri.
Komredi Kihwele ameweza kutoa Hati za Pongezi kwa Madiwani 38 wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa wakiwemo wa Vita Maalum na Wabunge, wa Jimbo la Isimani Mheshimiwa William Lukuvi na wa Jimbo la Kalenga Mheshimiwa Jackson Kiswaga.
“Kwa kasi hii ya utekelezaji wa Ilani hatuna cha kumlipa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zaidi ya kumuahidi ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika 2024”.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2022/2023 Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Veronica Kessy ameweza kuzungumzia wingi wa watu kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022 Halmashauri ina jumla ya watu 315,354 ikiwemo wanawake 161,798.
Pia ameweza kugusia hali ya watumishi na stahiki zao mbalimbali za kiutumishi na mambo mengine ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kuwa, hadi kufikia Juni 2023 zaidi ya kiasi cha Shilingi Bilioni 3.9 sawa na asilimia 99 ya makadirio ya bajeti ya mwaka zilikusanywa. Maendeleo makubwa ya huduma za elimu, maji, afya, barabara, umeme, uboreshaji wa kazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa na hali ya usalama katika Halmashauri.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Wakili Bashir Muhoja amesema, “nikiangalia timu yangu naona waliotoka ndani ya Iringa ni wachache, hivyo wengi tumetoka mbali na kuja kuhudumia wananchi wa Iringa. Uwepo na changamoto ni kawaida kwani penye mafanikio hapakosi changamoto, na kwamba tunazichukua kama fursa. Japo hatutaweza kwa asilimia 100 lakni tunajitahidi kwa kadiri ya uwezo wetu”.
Wakili Muhoja ameendelea kuseama kuwa, “watumishi wapo tayati kutekeleza Ilani hasa kwa kipindi hiki kabla ya uchaguzi. Tunashukuru kwa kuendelea kutusimamia na kutukosoa pale tunapokosea katika utendaji wetu wa kazi”
“Bado siku chache Darasa la Saba wafanye mitihani yao ya kuhitimu elimu ya msingi, ambapo itafanyika tarehe 13 -14 Septemba, 2023, hivyo tuwaombee”.
Kadhalika Wakili Muhoja ameongeza kusema kuwa, Hospitali ya Wilaya iliyopo Igodikafu imeanza kutoa huduma za upasuaji, na kwamba hivi karibuni tutapokea gari ya wagonjwa ili kurahisisha huduma.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa