Hatujakatazwa kuendeleza Mila Ambazo ni Nzuri na Rafiki - RC Dendego
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego amewataka Viongozi wa kidini, Kimila pamoja na Watanzania wote kurudisha na kuendelea kuzidumisha mila zetu kuanzia kwenye ngazi ya familia (malezi), shule pamoja na katika maisha ya kila siku.
Amesema Wazazi ni lazima kusema na watoto ikiwemo kuwakanya wanapokosea na sio kuwacha kutumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii kwani huko ndiko wanakoharibiwa na kuzalisha makatili wa sasa na baadae.
Ameyatamka hayo katika uzunduzi wa Kampeni ya Siku Kumi na Sita za Kupinga Ukatili wa Kijinsia na Watoto uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa (Siasa ni Kilimo) na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na Wilaya zote.
"Matukio ya kikatili yanaumiza, yanaumiza akili na yanaumiza mwili wakati mwingine kabisa yanapelekea baadhi ya watu kuwa na msongo wa mawazo na mwisho kupotelea huko".
Amesema pia katika siku hizi kumi na sita za kupinga ukatili amepanga kupita katika shule zote akiwa na Waandishi wa Habari kusisitiza kuhusu kutoa adhabu kwa wanafunzi pale wanapokosea.
"Sasa hivi wazazi tunawaogopa watoto, tunaona wanaharibika lakini tunaogopa kusema nao, wanashindwa kutueleza wanapokutana na dalili za ukatili kwa sababu hatujawajengea uwezo wa kukabiliana na viashiria fulani vya ukatili".
Aidha amesema vitendo hivi vya kikatili vimekuwa vikifanywa na watu wa karibu wakiwemo ndugu na kwa sababu wazazi hawapatikani nyumbani wanakuwa katika shughuli za utafutaji basi wajomba, baba wadogo na ndugu wengine hutumia mwanya huo kufanya vitendo hivyo vichafu.
"Na leo vitendo vingi vunafanyika nyumbani na watu wa karibu ambao wazazi wamewakaribisha na wanatumia nafasi hiyo kubaka, kulawiti watoto wetu".
Kadhalika amelitaka Jeshi la Polisi Mkoa Wa Iringa kuhakikisha ndani ya hizi siku kumi na sita wanakamilisha upelelezi wa mashauri yote ya ukatili ambayo yameripotiwa yaweze kukamilika na kushughulikiwa kulingana na sheria ili iweze kuwa mfano kwa jamii.
Naye Katibu Tawala Mkoa Mhandisi Leonard Robert Masanja amesema dhana ya ukatili ni pana sana na imekua ikianzia katika ngazi ya familia hivyo amewataka watu wote kuanza kupigana vita hivi na amesena itakua vyema kama itaanzia damuni yani kwa kuvichukia vitendo hivo.
"Matukio haya yanakwenda mbali zaidi mpaka mashuleni walimu wamekua wakibaka wanafunzi, hata Vyuoni pia wanawake wamekua wanyanyaswa kingono ili waweze kufaulu mitihani kadhalika Maofisini Wanawake wamekuwa wakiombwa Rushwa ya ngono ili wapate kazi hii haikubaliki". Amesema.
Ufunguzi wa Kampeni hizi umefunguliwa rasmi Novemba 25, 2022 na kutamatika Disemba 10 ikiwa na kauli mbiu isemayo "Kila Uhai Una thamani Tokomeza ukatili wa wanawake na watoto".
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa