Kamati ya Fedha Yampa Tano Muhoja,
Mhapa Asema ni DED wa Kipekee
Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango Halmashauri ya Wilaya ya Iringa wametoa sifa na pongezi nyingi kwa Mkurugenzi Mtendaji Wakili Bashir Muhoja kwa namna anavyosimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya Halmashauri.
Wajumbe wa Kamati hiyo ambao ni Waheshimiwa Madiwani wameonesha mahaba yao wazi wazi ya namna walivyofurahishwa na kupendezwa na kwa jinsi Mkurugenzi Mtendaji anavyofanya kazi kwa bidii na juhudi kubwa huku akiitekeleza miradi kwa ubora wa hali ya juu.
Hayo yamejiri tarehe 2 Februari wakati Kamati hiyo ilipokua katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo namna ilivyotekelezwa na kufanya tathmini ya pamoja kama kamati mama.
Katika pongezi hizo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Stephen Mhapa amesema kuwa Mkurugenzi Wakili Muhoja amekuwa kiongozi na mtendaji wa kipekee anaefanya kazi kwa ukaribu na Waheshimiwa Madiwani.
"Mimi nimefanya kazi na Wakurugenzi wengi sana lakini utendaji kazi wa Muhoja ni wa kipekee sana, yani ni mfuatiliaji na huo ndio ukweli".
Aidha amesema kuwa Muhoja amekuwa na maelezo ya kutosha kuhusu miradi yote inayotekelezwa bila kutegemea majibu kutoka kwa Wakuu wa Idara, huku akiifahamu miradi yote pamoja na matumizi ya fedha namna ilivyotumika.
"Mimi nasema nakupongeza sana Mkurugenzi, kazi tumeiona, madarasa, zahanati, vituo vya afya tumejenga na licha ya changamoto zote lakini umekua mvumilivu, Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, Mimi nakupongeza sana Muhoja".
Kadhalika Mhe. Mhapa amewapongeza wasaidizi wa Mkurugenzi yaani watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na amesema mchakamchaka wa Wakili Muhoja ni wa kipekee kwani akitoa kazi lazima aifuatilie na huo mchakamchaka ndio umesababisha maendeleo hayo. Aliongeza.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mhe. Methew Nganyagwa amempongeza Mkurugenzi Muhoja kwa usimamizi na ubora wa miradi hiyo aidha ameagiza kuandaliwe makala maalumu ili kuonesha ubora wa miradi ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Lumuli Mhe. Yohanes Mlusi ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo amempongeza Mkurugenzi Mtendaji na kusema kuwa ilikua ni kama ndoto kuwa na majengo ya kisasa yanayovutia kwa ubora hasa ukizingatia utekelezaji unafanyika kijijini kitu ambacho kwa kawaida ilikua ni kama haiwezekani.
"Mimi binafsi na wananchi wangu tunashangaa sana yani hatujawahi kuona madarasa ya malumalu, majengo ya ubora wa viwango vya juu, kwa kweli hongera sana Mkurugenzi". Amesema Mhe. Mlusi.
Shukrani na pongezi nyingi pia zimekwenda kwa Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mhandisi Nicco Kasililika ambae amekuwa mtendaji na msimamizi mkubwa wa miradi yote inayktekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Akijibu pongezi hizo Mkurugenzi Mtendaji Wakili Muhoja ameshukuru kwa kupewa pongezi hizo na kusema kuwa mafanikio yote haya ni kwa sababu ya ushirikiano anaoupata kutoka kwa Wahe. Madiwani na kuwaomba kuendelea kutoa ushirikiano pale wanapohitajika kwani Halmashauri ni ya watu wote.
Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa na Kamati hiyo ni pamoja na Mradi wa madarasa mawili yanayopatikana katika Shule ya Sekondari Muhwana, Kituo cha Afya Magulilwa, Jengo la Makao Makuu ya Halmashauri linalopatikana katika Kijiji cha Ihemi Kata ya Mgama, Ujenzi wa chumba kimoja cha darasa katika Shule ya Sekondari Lyandembela na Ujenzi wa Kituo cha Afya Kibena.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa