Kamati ya Ushauri ya Wilaya Yajadili Rasimu ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
“Bajeti imekaa vizuri na ni rahisi kutekelezeka, hivyo nawasihi kusimamia miradi kama ilivyopangwa na kutumia pesa kwa kadiri ya matumizi yalivyoainishwa”.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Veronica Kessy, wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) cha tarehe 15/02/2023 katika Ukumbi wa Siasa ni Kilimo kwa ajili ya kuchambua na kujadili Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024.
Awali akifungua kikao hicho ambacho Mwenyekiti ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mh. Kessy alikuwa na haya ya kusema,” kikao hiki ni kwa ajili ya agenda moja tu ambayo ni mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 kwa Halmashauri hii, hivyo nawasihi muwe watulivu na kuchangia mada”
Mhe. Kessy ameongeza kusema kuwa, “pamoja na kujadili Bajeti natoa nasaha zangu kwenu kuwa, nawasissitiza wananchi kupanda miti hasa kipindi hiki cha mvua. Ndani ya misitu wekeni mizinga ya nyuki ili muweze kuvuna asali, ambapo mwisho wa siku itaingiza kipato kwa jamii. Miti huongeza na kuvuta mvua, hivyo kufanya Bwawa la Mtera kujaa, ambapo litazalisha umeme bila tatizo”.
“Vichimbwe visima vifupi kwa ajili ya kufanya umwagiliaji wa mbogamboga kwani kilimo cha pembezoni mwa vyanzo vya mito ni tatizo na kufanya mito kukauka kwa haraka. Bustani za nyumbani ni nzuri sana hasa kwa lishe na kutatua gharama ndogondogo. Pamoja na haya usafi wa mazingira ni muhimu katika maeneo yetu”. Amesema Mh. Kessy.
Aidha Mheshimiwa Kessy hakuacha kusisitiza suala la wanafunzi wanaotakiwa kuanza Kidato cha Kwanza, na kusema kuwa kama mtoto hajaripoti hadi sasa mzazi/mlezi lazima achukuliwe hatua na atoe sababu za kwa nini mwanafunzi hajaripoti, na kuhitaji hadi kufikia tarehe 20/02/2023 wanafunzi wanaohitaji kuanza Kidato cha Kwanza wawe wamefikia 95%.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Iringa, Comredi Costatino Kihwele amemshukuru Mkuu wa Wilaya Mh. Kessy na kumuhakikishia usalama wa Wilaya na kwamba Chama kipo tayari kupokea maelekezo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Stephen Mhapa amesema, anamshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Mh. Kessy kuja kuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, na kuahidi kutoa ushirikiano katika utendaji kazi.
Baada ya hotupa fupi ya viongozi hao Afisa Mipango wa Wilaya Ndugu. Xavery Luyagaza, aliwasilisha Mapendekezo ya Rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa