Katibu Mkuu CCM Taifa Aleta Neema kwa Wananchi
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Taifa Ndugu Daniel Chongolo aliagiza kujengwa kwa mabweni katika shule ya sekondari Tanangozi, Pamoja ukarabati wa barabara zinazozunguka vijiji vya Udumuka – Mfukulembe, Ifunda- Udumuka, Ikwega – Udumuka na Bandabichi – Ifunda Tech, Pamoja na Wenda hadi Hospitali ya Mt. Theresa.
Ndg. Chongolo alisema hayo wakati wa ziara yake ya siku mbili katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ambayo ilianza Mei 29 hadi 30, 2023, kwenye Majimbo yote mawili ya Kalenga na Isimani, ambapo alitembelea na kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi wa madarasa na mabweni shule ya sekondari ya wasichana Ifunda, upandaji wa vifaranga katika bwawa la Kata ya Masaka, pia alikagua ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Lyamgungwe.
Aidha May 30, Ndugu Chongolo alikagua barabara ya Kising’a-Ilambilole- hadi Isimani Tarafani, pamoja na kuzindua mradi wa maji uliopo katika Kijiji cha Chamndindi Kata ya Nyang’oro, sambamba na ukaguzi wa mfereji wa umwagiliaji wa Mkombozi uliopo katika Tarafa ya Pawaga.
Ndugu Chongolo katika ziara yake aliweza kuwatembelea baadhi ya Mabalozi wa Shina kwa lengo la kuongea nao na kutatua changamoto zao, ikiwa ni Mjumbe wa Shina Namba 7 wa Kijiji cha Ilambilole ambaye amekuwa akiishi katika nyumba ya kupanga, hivyo kuamriwa ajengewe nyumba yake. Katika zoezi hilo Ndugu Chongolo aliweza kununua kiwanja na kuanza ujenzi wa nyumba hiyo mara moja.
Sambamba na hayo Katibu Mkuu huyo wa CCM Taifa, aliwataka viongozi wa Chama kuanzia ngazi ya Shina hadi Wilaya kuwahimiza wananchi wajiunge na chama hicho ili Ilani ya maendeleo iweze kutekelezwa ipasavyo, kutokana na chama hicho kushika hatamu.
Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi, Bi. Sophia Mjema, alisema kuwa Sekta ya Afya imezindua mfumo wa M-MAMA ambao utakuwa maalumu kwaajili ya kuwasaidia akinamama kupata rufaa kutoka kwenye Zahanati kwenda Vituo vya Afya au Hospitali ya Wilaya, kwa kupiga simu ili waweze kuletewa gari ya wagonjwa.
Pia, Bi. Mjema amesema kuwa, mfumo huo utasaidia kupunguza vifo vya akimama na watoto wachanga kutokana na kukumbwa na changamoto za mara kwa mara za kiafya hususani kipindi cha ujauzito na uzazi.
Hata hivyo, Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wa CCM, aliwataka wakazi wa Mkoa wa Iringa, kuacha kuuza mazao ya chakula hovyo ili waweze kukabiliana na baa la njaa, ikiwa ni pamoja na kuzalisha chakula chenye virutubusho kutokana na kuwepo kwa takwimu za juu za udumavu Mkoani humo.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa na Wilaya ya Iringa, Ndugu. Daud Yasin Mlowe, aliwashukuru viongozi wa chama hicho kuamua kufanya ziara katika Halmashauri hiyo, ili kujionea utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo na kuahidi kusimamia Ilani ya Chama hicho ili nchi iweze kuwa na maendeleo endelevu.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa