Kiasi cha Shilingi za Kitanzania Bilioni 60.2 zapitishwa Katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024
Baraza la Maalum la Madiwani lapitisha Kiasi cha Shilingi Bilioni 60.2 kuwa Bajeti ya Halmashauri kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024.
Bajeti hiyo ambayo imekuwa na sura tofauti na kipindi kilichopita, waheshimiwa Madiwani wameipitisha bila kupinga kutokana na umbile lake, kwani imebeba mambo mengi ya msingi hasa miradi ya maendeleo.
Pamoja na kusomwa bajeti ya Halmashauri pia Taasisi nyingine ambazo zipo chini ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa yaani Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) nao walipata nafasi ya kusoma bajeti zao ambazo zitatekelezwa kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha 2023/2024.
Kwa upande wa TARURA wameweza kuweka bajeti ya Shilingi Bilioni 40.089 kwa ajili ya kutekeleza miradi yake, na RUWASA imesomwa bajeti ya Shilingi Bilioni 5.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Akitoa hotuba yake fupi Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Veronica Kessy amesema, anampongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kwa kufanya mchakato wa bajeti hii na kukamilika hatimaye kusomwa na kukubalika.
Aidha Mheshimiwa Kessy hakuacha kugusia suala la wanafunzi wa Kidato cha Kwanza kuripoti shuleni na kutoa siku saba kuanzia tarehe ya leo, wanafunzi wote wawe wameripoti Kidato cha Kwanza, na kwamba kama kuna mtoto ambaye amefichwa au kutoroshwa basi mzazi au mlezi achukuliwe hatua.
Aidha Mheshimiwa Kessy amesisitiza kwa kusema kuwa, “Watendaji wote wa Kata/Vijiji mkishirikiana na Waheshimiwa Madiwani fanyeni ukaguzi nyumba kwa nyumba kuona kama kuna mtoto ambaye hajaripoti shule”.
Mheshimiwa Kessy ameongeza kusema kuwa, utoaji wa chakula shuleni ni lazima sana, kwani itamfanya mtoto aweze kusoma kwa morali kwa sababu atakuwa na uhakika wa kupata chakula cha mchana shuleni. Ameongeza kusema kuwa, wazazi/walezi ni lazima wachangie chakula shuleni, kuwepo na kamati maalumu ya mapokezi ya chakula.
Mheshimiwa Kessy ameendelea kusema kuwa, jambo la lishe ni muhimu kulitekeleza kwani ni agizo na ni agenda ya Serikali Kitaifa. Kila kipindi cha Robo lazima fedha ziidhinishwe ili kutekeleza Afua za Lishe. Mhe. Amempongeza Mkurugenzi Mtendaji kwa kutekeleza Afua za Lishe kwa mwaka wa Fedha 2022/2023 kwa kutekeleza mpango huu wa lishe kwa 100%.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Isimani Mheshimiwa William Lukuvi amewapongeza watendaji wa Halmashauri kwa kufanya kazi vizuri wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Wakili Bashir Muhoja.
Mheshimiwa Lukuvi ameongeza kusema kuwa, tatizo la Halmashauri hiyo ni mapato kwani ina vyanzo vichache. Hivyo ametoa wazo la kuanzisha vyanzo vingine ambavyo vitaweza kuingizia Halmashauri mapato kama kuwekeza na kukodisha mashamba ya mpunga, mashamba ya miti ambayo itatoa fursa hata kwa kizazi cha baadaye.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Stephen Mhapa amelipongeza Baraza la Madiwani kwa kutoa michango yao na kuhitimisha Mkutano wa Baraza vizuri. Pia amemshukuru Mheshimiwa Lukuvi kwa kuungana na Baraza kwani ni mwakilishi mzuri Bungeni kwa kutetea maslahi ya Halmashauri.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa