Kombe La MBOMIPA Larindima Kwenye Jumuiya Ya Uhifadhi
Na. Zaitun Omary,
Iringa DC.
Shirika la Uhifadhi Tembo Kusini mwa Tanzania (Southern Tanzania Elephant – STEP) kwa kushirikiana na Shirika la Uhifadhi Wanyama Walao Nyama (Lion Landscape), wameandaa Bonanza la Mpira wa Miguu kwa Jumuiya za Uhifadhi kuanzia tarehe 30/10/2022 hadi 11/11/2022 katika Kata ya Idodi kwenye vijiji vya Mapogoro na Tungamelenga.
Lengo la Bonanza hilo ni kwa ajili ya kutoa elimu jumuishi kwa jamii juu Uhifadhi wa Wanyama pori na uhifadhi wa mazingira katika vijiji vinavyozunguka mbuga. Mashirika haya ni wadau wa Uhifadhi Mbuga ya Ruaha, hivyo kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa ajili ya kutoa elimu hiyo.
Akizungumza katika ufunguzi wa bonanza hilo, Mratibu na Msimamizi wa miradi ya STEP Ndugu Godfrey Nyangalasa amesema, “tumeandaa bonanza hili kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii juu uhifadhi wa wanyamapori na utunzaji wa mazingira, na jamii ione umuhimu na itoe ushirikiano wa uhifadhi wa Wanyama pori na mazingira”.
Bwana Nyangalasa ameendelea kusema kuwa, “Tumeshirikiana na Wadau wenzetu wa Uhifadhi wa Wanyama Walao Nyama (Lion Landscape) ili kuleta ufanishi mkubwa katika jambo hili la uhifadhi”.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Idodi Mheshimiwa Julias Mbuta amesema, “tupo hapa kwa nia moja tu ya kutoa elimu kwa jamii juu ya uhifadhi wa wanyama na mazingira. Bonanza hili litaendelea hadi tarehe 11/11/2022 katika vijiji vyote vinavyozunguka Hifadhi – Mbuga, na mwisho wa siku washindi watapata zawadi, hivyo chezeni kwa furaha”.
Naye Afisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bi. Fatuma Juma alikuwa na haya ya kusema, “kutunza mazingira ni fahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadae. Bonanza litaendelea katika vijiji 22 vya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ambapo ni Mahuniga, Makifu, Kitisi, Mafuluto, Malinzanga, Isele, Magombwe, Kinyika, Kimande, Itunundu, Mbuyuni, Mkombilenga, Mboliboli, Mbugani, Ilolo, Magozi, Ukwega na Luganga. Baada ya mechi kutakuwa na sinema inayofundisha jinsi ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira na Wanyama”, amesema Bi Fatuma.
Baada ya ufunguzi huo ulifuatiwa na mchuano mkali wa mechi ya mpira wa miguu kati ya Kijiji cha Tungamalenga na Kijiji cha Mapogoro, na mshindi amepatikana Kijiji cha Mapogoro kwa kufunga goli moja. Baada ya mechi jioni hiyo wananchi waliburudika kwa kuangalia sinema inayofundisha jinsi ya kuhifadhi Wanyama Pori na mazingira.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa