DC Moyo Awataka Wananchi Kuendelea Kusimamia Haki za Mtoto
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Mohamed Moyo amewaagiza wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kuhakikisha wanasimamia haki zote za msingi za mtoto.
Mhe. Moyo ameyasema hayo leo Jumatano Juni 15, 2022 wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Kising’a katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyoadhimishwa Kiwilaya katika Kata hiyo Viwanja vya Kanisa la Kilutheri Tanzania K.K.K.T Kising’a.
Amesema ulinzi wa mtoto unajumuisha hatua zote za kisheria, kiutawala kijamii, na kielimu za kuzuia na kupinga ukatili wa kinyonyaji,, utelekezaji na unyanyasaji dhidi ya watoto, utumikishaji kwa maana ya ajira za utotoni, amewaomba wazazi kukemea mambo hayo kwani mtoto anahitaji ulinzi na usalama pamoja na haki ya kupewa elimu.
Lakini pia amezungumzia suala la umuhimu wa watoto kupata haki zao na kusema kuwa mtoto ana haki kuanzia kwenye tumbo la mama yake, hivyo wazazi wamehimizwa kumpatia mtoto haki zake zote za msingi.
“Tumpe mtoto nafasi ya kukua, ukatili kwa mtoto una madhara kwa mtoto kihisia, kitabia na kimwili watoto wanaotendewa ukatili hukabiliwa na athari ya kufanya vibaya mashuleni, vitendo vya kikatili pia ndio sababu ya watoto wengi kukimbia majumbani na kwenda kuishi mitaani.”
Lazima kama wana Iringa, Wazazi mambo haya tuyakemee kwa nguvu zote, masuala ya watoto kufanyiwa ukatili wa kijinsia halafu wazazi wanasema wanamalizana bila kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria lazima tuyakemee na tuyakatae kwa nguvu zote, kwani bila kufanya hivyo matendo haya hayatakoma. Ameongeza
Amehimiza pia mshikamano kati ya wazazi, viongozi wa serikali na viongozi wa dini katika kupigania haki za mtoto na kupinga vitendo vya ukatili. Pia amesema kusiwepo na agenda za kikatili wakati wa maadhimisho tu bali liwe ni jambo la kulijadili muda wote.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mhe. Stephen Mhapa amewashukuru wazazi na waalimu kutoka Kata ya Kising’ga kwa malezi mazuri wanayowapatia watoto na kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi, aidha amemshukuru Mkurugenzi na Wataalamu wote waliohakikisha kuwa maadhimisho haya yanafanikiwa.
“lakini kipekee pia niwashukuru wenzetu wa Mashirika yote, na nikiwa kama Msimamizi Mkuu wa Halmashauri niseme sisi tunawashukuru Mashirika yote kwa sababu yanafanya kazi kwa niaba ya Serikali, kazi mnayofanya hiyo tulipaswa sisi kufanya, Mungu awabariki sana na atawaongezea siku nyingi za kuishi na mafanikio mengi katika shughuli zenu mnazozifanya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Iringa Vijijini Mhe. Costantino Kihwele amesema wito wa Chama cha Mapinduzi ni kuhakikisha watoto wanalindwa kufa na kupona na suala hili si la jeshi la polisi pekee bali ni la wadau wote lazima tushirikiane kumlinda mtoto, amewaomba wananchi kuacha tabia ya kumalizana vichochoroni.
Aidha ameagiza kuwa kila mzazi ahakikishe anatoa mchango wa chakula ili mtoto apate chakula akiwa shuleni kwani ni moja ya haki anayotakiwa kupewa mtoto. Lakini pia ameahidi kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi kutoa ushirikiano katika malezi na makuzi sahihi na bora kwa mtoto.
Diwani wa Kata ya Kising’a Mhe. Ritha Mlagala ambaye maadhimisho haya yamefanyika katika Kata yake ya Kising’a, amewashukuru wananchi wote waliojitokeza katika maadhimisho hayo kadhalika amewashukuru Mkurugenzi na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa kuhakikisha kuwa maadhimisho haya yanafanyika na kufana katika Kata ya Kising’a.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja amesema kuwa, kuna tabia illiyozuka ya ubakaji na tayari ameshapokea kesi mbili za watu wanaovamia watoto shuleni na kuwabaka, hivyo amewaagiza Wataalamu kutoka Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Jamii, Elimu Sekondari na Msingi kuhakikisha kuwa wanahamasisha jamii kuendelea kuwa walinzi wa watoto pindi waendapo shuleni na warudipo majumbani.
Kwa upande wa Dawati la Jinsia Wilaya Inspekta Msaidizi Lydia Sospeter amesema kuwa, sababu zinazopelekea watu kufanya ukatili ni uelewa mdogo wa sheria, lakini kitu kingine ni mila na desturi zetu, kwamba wazazi wengi wamekuwa wakiwakatiza watoto masomo na kuwapeleka kuolewa pia imani za kishirikina zinachangia sana.
“Ninachowasihi ni kufanya kazi kwa sababu inaonekana kuwa matukio mengi ya ukatili yanatekelezwa na watu ambao hawana kazi za kufanya, hivyo wananchi wote watakiwa wafanye kazi ili kujiepusha kusababisha vitendo vya ukatili kwa watoto .”
Ulevi uliopindukia pia ni chanzo cha ukatili hivyo wazazi nawahimiza kuacha tabia ya ulevi hasa nyakati za msimu wa ulanzi kwani ni kichocheo kikubwa cha ukatili kwa watoto na watu wazima. Pia nawahimiza vijana mjitahidi kujifunza kutongoza wasichana ili msijiingize katika vitendo vya ubakaji. Ameongeza.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bi. Saumu Kweka amewashukuru Mashirika mbalimbali yaliyojitokeza kutoa ushirikiano ili kufanikisha Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika iliyoadhimishwa Kiwilaya katika Kata ya Kising’a viwanja vya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (K.K.K.T) Kising’a.
Mashirika hayo ni pamoja na Compassion, Lyra, Afya Plus, Nyumba Yetu, SOS, ASAS, World Vision, Call Afrika, na wengine wengi.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa