Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani Yafana Iringa
Kila ifikapo Desemba Mosi dunia huadhimisha Siku ya UKIMWI ili kueneza ufahamu wa ugonjwa wa UKIMWI unaosababishwa na uambukizi wa virusi vya UKIMWI. Ni kawaida kuwa na ukumbusho wa siku hii ili kuikumbusha jamii kuhusu ugonjwa huu na pia kuwajali watu ambao wamefariki kutokana na VVU / UKIMWI.
Kwa Serikali ya Mkoa wa Iringa imeadhimisha maadhimsiho haya katika Halmashauri ya Wilaya yaIringa Kata ya Mseke Kijiji cha Ugwachanya na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Mkoa, Wilaya, Halmashauri, Wadau, Viongozi wa Dini pamoja na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akimuwakilisha Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego, Katibu Tawala Mkoa Mhandisi Leonard Robert Masanja amesema maadhimisho ya siku hii yanatoa fursa kwa Serikali, Wataalamu katika sekta mbalimbali, Wanasiasa Viongozi wa Dini na Wananchi kuungana pamoja na kuimarisha juhudi za kudhibiti janga la Virusi vya UKIMWI.
Amesema kauli mbiu ya mwaka huu ni Imarisha Usawa hivyo amesisitiza utoaji wa huduma bora za tiba na matunzo bila unyayapaa na ubaguzi kwa wapokeaji wa huduma hizo yaani ndugu zetu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI.
“Kauli mbiu hii pia ikafanye kazi vizuri kwa wale watu wapya wanaotambulika na kuunganishwa na huduma hizo kwa mara ya kwanza katika vituo vyetu ili waweze kuwa wafuasi bora wa huduma”
Nimefarijika sana na muitikio wenu katika maadhimisho haya kwani inaonesha uwajibikaji wenu na ushiriki katika shughuli za kudhibiti maambuzi mapya ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI mkoani kwetu. Ameongeza.
Aidha amesema jambo kubwa kwa sasa ni utekelezaji wa afua mbalimbali ambazo zitatufikisha kwenye kizazi ambacho hakina maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI, hakina unyanyapaa na hakina vifo vinavyotokana na UKIMWI ifikapo mwaka 2030 kama malengo ya dunia yanavyosema.
“Ni ukweli usiopingika kuwa kila mmoja wetu kwa namna moja ama nyingine ni muathirika wa janga hili, kama ndivyo kwa nini tusichukue hatua kama jamii kwa kuwajibika ili tuweze kuepusha vizazi vyetu vijavyo na athari hizi”.
Pia amesema Serikali ya Mkoa itahakikisha inaimarisha mahusiano na wadau na kuendelea kujengea uwezo vituo ili kuweza kutoa huduma bora za tiba na matunzo kwa jamii na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi ya maambukizi.
Aidha ametoa maagizo kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuendelea kutengea bajeti za mipango na shughuli za kuendeleza huduma za VVU na UKIMWI ndani ya vituo vya Halmashauri ili kuwa na huduma endelevu.
Sambamba na hayo pia amewaagiza Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri kuendelea kusimamia kikamilifu shughuli zote za mapambano dhidi ya UKIMWI katika Wilaya na Halmashauri.
Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ndani ya mkoa katika utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI ni kuongezeka kwa idadi ya vituo vinavyotoa huduma za tiba na na matunzo (CTC), kuongezeka kutoka vituo 63 mwaka 2017 hadi kufikia vituo 184 mwaka 2022.
Pia kuimarika kwa upatikanaji wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba kwenye huduma za VVU na UKIMWI ambapo kumesaidia kuondoa malalamiko kwa walengwa na hali sasa hivi ni bora zaidi.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa