Maafisa Ugani Wamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Kuwapatia Pikipiki
“Azimio la Mwaka 1972 la Siasa ni Kilimo lilitolewa Mkoani Iringa na Baba wa Taifa Mwal. Julius Kambarage Nyerere, lilikuwa na maana kubwa kwa Mkoa huu, akimaanisha ni Mkoa wa uzalishaji. Hivyo pikipiki hizi mkazitumie vizuri kwa kuwatembelea wakulima na kutatua kero zao mkiwa shambani, ili ikasadifu na Azimio hili”
Kauli hii imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mheshimiwa Halima Dendego alipokuwa katika hafla fupi ya kukabidhi pikipiki kwa Maafisa Ugani zaidi ya 230 wa Mkoa wa Iringa. Hafla hiyo imefanyika leo tarehe 28/02/2023 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Mheshimiwa Dendego ameendelea kusema kuwa, Mkoa wa Iringa unazalisha chakula kwa wingi, kwani ni moja ya sifa kubwa katika Mkoa huu kwa Tanzania. Hivyo kuwaasa Maafisa Ugani hao kuwa, hakuna visingizio tena vya kushindwa kuwafikia wakulima na kuweza kutatua kero zao huko shambani.
Pia Mheshimiwa Dendego amewasisitiza Maafisa Ugani hao kuwa, pikipiki hizo wasitumie katika mambo yao binafsi, bali watumie kama kitendea kazi.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa Mhandisi Leonard Masanja amesema, anamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa vyombo hivi ili viweze kuwasaidia Maafisa Ugani katika kazi zao, na kufanya kazi kwa bidi.
Awali akitoa taarifa fupi ya mapokezi ya pikipiki hizo Msaidizi wa Katibu Tawala Sehemu ya Uchumu Ndugu Elias Luvanda amesema, Mkoa umepokea pikipiki 230, japo kuna Maafisa Ugani 231 na mahitaji yakiwa 444 na kufanya upungufu wa Maafisa Ugani 214, vituo 18 vya kutolea huduma za ugani. Pamoja na mapokezi ya pikipiki hizo, Mkoa pia umepokea pawatila 1.
Ndugu Luvanda ameendelea kusema kuwa, pamoja na mafanikio hayo bado kuna changamoto za, vituo vya kutolea huduma vinaakiwa kufanyiwa ukarabati, uhaba wa Maafisa Ugani, baadhi ya Maafisa Ugani kukasimishwa Utendaji Kata au Kijiji na Halmashauri kutokuwa na bajeti ya kutosha.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri, ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Bi. Lucy Nyalu amewasisitiza Maafisa Ugani wakatumie vyombo hivi kama ilivyopangwa na kwamba watapimwa kwa kiwango cha uzalishaji katika maeneo yao ya kutolea huduma.
Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa zimepokelewa pikipiki 78 kwa ajili ya Maafisa Ugani.
Naye Afisa Usafirishaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Ndugu Haward Thom akiwa anatoa maelekezo kwa Maafisa Ugani namna ya kutumia vyombo vya moto amesema, kwanza lazima mtu awe na leseni, pia ajue kuendesha chombo hicho.
Kabla ya kuwakabidhi vyombo hivyo na kuondoka navyo Ndugu Thom amawataka Maafisa Ugani hao kujiandaa katika kuvitumia, na kwamba ametoa muda wa mwezi mmoja kila Afisa Ugani aliyepewa pikipiki awe amekamilisha taratibu na vigezo, yaani leseni na kuelewa namna ya kutumia chombo hicho.
“Natoa mwezi mmoja kama tulivyokubaliana kila mtu awe amepata leseni na anajua jinsi ya kutumia pikipiki. Mnatakiwa kwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili mkakate leseni”, Amesema Thom.
Ndugu Thom ameendelea kuwaasa Maafisa Ugani hao kuwa, wanatakiwa kuwa na tahadhari wakati wakitumia vyombo hivi, kwani vikiharibika au kupotea watalazimika kutumia mishahara yao kwa ajili ya kununua chombo kingine. Pia hairuhusiwi kubadilisha muonekano wa chombo kwani ni mali ya Serikali.
Pamoja na zoezi la kukabidhi pikipiki Mheshimiwa Dendego amepokea msaada kutoka kwa Wadau mbalimbali kwa ajili ya ajali ya moto iliyotokea katika Shule ya Sekondari St. Michael ambapo liliungua bweni la wasichana.
Msaada huo ni mablanketi, mashuka, sabuni na taulo za kike. Mheshimiwa Dendego amevishukuru Vyombo vya Habari kwa kuonesha matukio ya ajali hiyo, na kuonekana na Wadau ambao wanaendelea kutoa msaada.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa