Mabadiliko ya Kutokomeza Vitendo vya Kikatili Yanaanza na Mimi na Wewe - DC MOYO
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Mohammed Moyo amesema mabadiliko ya kutokomeza vitendo viovu vya kikatili katika jamii zetu vinapaswa vianzwe na mtu mmoja mmoja ndipo tutaweza kupiga hatua za kupunguza au kuondoa vitendo viovu katika jamii.
Amesema kwa kufanya hivyo kutapelekea kuwa na taifa ambalo linajali utu,haki na uhai wa wanawake na watoto, Ameyasema hayo katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Wanawake na Watoto yalioadhimishwa Kihalmashauri katika Kijiji cha Ikuvilo Kata ya Luhota.
"Tatizo la ukatili wa kijinsia lipo na waathirika wakubwa ni wanawake na watoto, kwa mfano takwimu zilizopo katika Halmashauri yetu mwaka 2021/2022 inaonesha kuwa ukatili unaochukua nafasi kubwa ni pamoja na ukatatili wa kimwili, kingono pamoja na utekelezaji wa familia".
Licha ya kuwa waathirika wakubwa ni wanawake lakini pia Mhe. Moyo amesema kuna wanaume wanaofanyiwa ukatili na wanashindwa kutoa taarifa kwa sababu wanaogopa kujulikana kutokana na unyanyapa uliotokana na mila potofu.
"Naomba niwaeleze kuwa kama usiri huu ukiendelea tatizo halitapungua, kila mtu anatakiwa kuhakikisha anapambana na ukatili wa aina yoyote ili ili kifikia jamii iliyostaarabika, inayolenga kujali utu na haki ya mtu".
Aidha ametoa wito kwa jamii na kwa kila mtu anaefanyiwa ukatili bila kujali jinsi yake au ameona na kushuhudia ukatili ukifanyika mahali atoe taarifa kwenye mamlaka husika au kupiga simu namba 116.
Amesema pia katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa zimeundwa kamati za ulinzi na usalama kwa mtoto katika vijiji 134, kata 28 na ngazi ya wilaya ambazo zitasimamia kwa ukaribu sana masuala ya kikatili na ulinzi kwa mtoto.
"Majukwaa ya wanawake 27 yameanzishwa, Mabaraza ya Watoto ngazi ya Wilaya Kata 27 na Vijiji 131, Vikundi vya malezi vya watoto katika kila Kata lakini pia Serikali imetoa mafunzo kwa wataalamu wetu wa afya, Maendeleo ya Jamii, Elimu na Ustawi wa Jamii ili kushughulikia matukio ha kikatili".
Aidha amesema kuwa umuhimu wa kuwashirikisha wanawake katika nafasi mbalimbali ili kutoa fursa sawa katika kumiliki mali Halmashauri imetekeleza mpango wa hati miliki za kimila ambapo zaidi ya wanawake elfu kumi wamemilikishwa ardhi.
Juhudi nyingine ni kiwahamasisha wanawake kijishughulisha na shughuli za kiuchumi ili kuwa na maisha bora na kuwaondoa katika dhana potofu ya utegemezi, kwa kuwawezesha mikopo ya wanawake ambapo kwa mwaka 2021/2022 jumla ya Tshs. 178,600,000/= kwa vikundi thelathini ikiwa ni wanawake 353.
Mhe. Moyo ametoa rai kwa Viongozi wa Vijiji na Vitongoji kuwa katika masuala yote yanayohusu ukatili ya kijinsia yashughuliliwe na polisi tu na sio viongozi wa vijiji au vitongoji, kutokana na kuwa na baadhi ya watendaji na viongozi amabo sio waaminifu wana tabia ya kumalizana woa kwa wao na ikigundulika basi mashtaka yatafunguliwa.
Ametoa rai pia kwa wananchi kuona umuhimu wa kuwa mstari wa mbele katika kupinga vitendo vya ukatili katika jamii hususani kwa kutoa taarifa za matukio ya ukatili ili kuiwezesha serikali kutambua na kuona ukubwa wa tatizo na kuweka mikakati ya kukabiliana na vitendi vya kikatili.
Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili duniani yalianza mwkaa 2006 yakiwa na lengo la kupinga ukatili wa kijinsia yaani ukatili wa kipigo, kingono, kutelekezwa, Kisaikolojia na ukatili wa wanawake na watoto wa kike kunyimwa fursa ya elimu, uongozi, haki ya umiliki wa mali, nafasi za uongozi nakadhalika.
Aidha maadhimisho haya huzinduliwa kila tarehe 25 novemba na kuhitimishwa kila tarehe 10 Desemba kwa kutekeleza kazi mbalimbali ikiwemo kutoa elimu ya jinsia kwa jamii, kusaidia na kuwafikia wahanga wa ukatili wa kijinsia pamoja na maadhimisho ya Siku ya UKIMWI.
Maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili kwa mwaka huu yanaongozwa na Kauli mbiu isemayo; "Kila Uhai Una Thamani, Tokomeza Ukatili na Mauaji ya Wanawake na Watoto".
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa