Timu ya Wawezeshaji Mafunzo kutoka TASAF yawanoa kwa Siku sita Wawezeshaji wa Halmashauri (W) Iringa
Na Ofisi ya Habari na Uhusiano
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja amefanya ufunguzi wa Mafunzo kwa wawezeshaji wa Mamlaka za maeneo utekelezaji kuhusu maandalizi, utekelezaji na Usimamizi wa Miradi ya kutoa ajira za muda chini ya mpango wa kunusuru kaya maskini - TASAF awamu ya tatu kipindi cha pili.
Timu ya wawezeshaji wa mafunzo kutoka TASAF, wawezeshaji wa kitaifa ambao ni wataalamu kutoka Halamashauri mbalimbali wamefika kutoa mafunzo hayo kwa lengo la kuwasaidia wawezeshaji kutoka Halmashauri juu ya mbinu na namna ya kuwasaidia wananchi katika kusimamia shughuli za miradi ya kutoa ajira za muda katika ngazi ya Vijiji.
Akifungua Mafunzo hayo ya siku sita, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja amesema mafunzo hayo ni muhimu na kila mmoja aliepata nafasi ya kuteuliwa kushiriki mafunzo hayo anastahili, hivyo wote kuwa makini katika kipindi chote cha mafunzo
"Natambua kuwa wote mko hapa kwa vigezo sahihi, uko hapa kwa sababu unastahili hivyo sitarajii uje ututhibitishie kuwa tulikosea kukuteua ninaomba muwe makini kwa kipindi chote cha mafunzo".
Ameongeza kwa kusema kuwa, mafunzo hayo ni muhimu sana kwani washiriki hao wakimaliza mafunzo watatakiwa wakawaongoze wananchi kuibua na kusimamia miradi mbalimbali ya kutoa ajira za muda katika Kata na Vijiji ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Kadhalika amewataka washiriki wote wa mafunzo kuwa makini katika kipindi chote cha mafunzo watakayopatiwa na wawezeshaji waliofika kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo na kuuuliza pale wanapokuwa hawajaelewa ili kusaidia kufanyika kwa kazi nzuri na yenye ufanisi kwa hapo baadae.
"Matunda ya mafunzo haya tutayaona katika vituo vyenu vya kazi, sasa kama utashindwa kuelewa vizuri utashindwa kuwajibika vizuri hapo baadae."
Akisoma hotuba kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga, Bi. Godliver Mvanda amesema, utekelezaji wa mpango huu unafanyika katika Mamlaka zote za maeneo ya utekelezaji za Tanzania Bara na Zanzibar na unatarajia kuzifikia kaya milioni moja na laki nne na nusu zinazokadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni saba kote nchini, hii ikiwa ni nyongeza ya kaya laki tatu na nusu ikilinganishwa na kipindi cha kwanza.
Ameongeza kwa kusema lengo kuu la mafunzo haya ni kujenga uelewa wa pamoja kwa wawezeshaji wa mamlaka za maeneo utekelezaji kuhusu uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa miradi yenye tija inayokidhi viwango vya kisekta na ubora unaokubalika.
“Ni matumaini yangu kuwa mtayapa umuhimu mkubwa mafunzo haya kwa kushiriki kikamilifu kwa siku zote sita zilizopangwa”. Alihitimisha.
Mwenyekiti wa mafunzo hayo Ndugu Lefdedy J. Msamba ambae ni Afisa Umwagiliaji amesisitiza washiriki kushiriki kikamilifu kuuliza maswali endapo hawajaelewa au kuna utata ili kuelewa na mwisho wa siku kazi nzuri ifanyike katika maeneo ya kazi.
Aidha amewataka washiriki na wawezeshaji kuzingatia muda ili mambo yaweze kwenda kama yalivyopangwa na pia kutaka ushirikiano kati ya washiriki na wawezeshaji.
Akizungumza katika mafunzo hayo Bi Agatha Lugome ambae ni Mratibu wa Mpango TASAF wilaya amesema anatarajia mafunzo haya yatasaidia kuwajengea uwezo washiriki hao na kuwasaidia wananchi katika usimamizi wa uibuaji wa miradi mbalimbali ya kutoa ajira za muda chini ya mpango wa kunusuru kaya maskini.
Kikao kazi hiki kinafanyika kwa mara ya kwanza katika eneo hili la mamlaka ya utekelezaji katika mzunguko wa pili wa utekelezaji wa miradi kwa mwaka 2022/2023.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa