Mafunzo ya Utoaji Mikopo 10% Yatolewa
Serikali baada ya kujiridhisha na namna bora ya utoaji mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu ya 10%, sasa yaja na njia mpya ya kutoa mikopo hiyo.
Kwa kuzingatia usawa wa utoaji mikopo hiyo sasa Serikali itatoa mikopo hiyo kupitia mfumo na siyo kwa njia ya benki kama ilivyokuwa hapo awali, ili kubaini vikundi halisi vitakavyokopa.
Akifungua mafunzo hayo kwa Maafisa Maendeleo wa Kata Oktoba 01, 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Ndugu Robert Masunya amesema, “nawasihi sana mkasimimie vizuri na kila mtu apate haki katika mikopo hiyo. Sasa hivi utoaji mikopo umebadilika kutokana na changamoto zilizojitokeza awali, na sasa tutatumia mifumo. Hivyo nawaomba kuleta vikundi vyenye sifa ili kuepukana na udanganyifu”
Ndugu Masunya ameendelea kusema, “endeleeni kukusanya madeni ambayo bado hayajalipwa ili kuwapa nafasi wengine waombe mikopo hiyo. Pia endeleeni kutumia fedha hizo kwa uaminifu na uadilifu”.
Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bi. Saumu Kweka, amewaomba Maafisa Maaendelo hao kuendelea kufuatilia vikundi ambavyo havijarejesha mikopo ili kuwapa nafasi ya kukopa tena. Pia amewahimiza kusimamia na kuwatembelea Kaya masikini na wenye mazingira magumu ili kujua hali zao na kuwahimiza kula chakula cha lishe bora.
Kadhalika, amewataka kuwatambua wanufaika wote wa TASAF ili waweze kufungua akaunti, mara ifikapo muda wa kupatiwa fedha kwa ajili ya kujikimu basi fedha hizo ziwekwe kwenye akaunti zao.
Maafisa Maendelo hao wamekumbushwa mambo mengi katika uboreshaji wa majukumu yao ya kila siku na kufanya kazi kwa bidii. Pia kutoa taarifa pale inapotokea changamoto katika eneo lake la kazi.
Mafunzo hayo yanatolewa kuanzia Oktoba 01-05, 2024 katika ukumbi wa Halmashauri Ihemi.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa