MHE. LUKUVI APOKEA WAJUMBE WA BODI YA HELEN KELLER INTERNATIONAL
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. William Lukuvi, amewapokea na wajumbe wa Bodi wa Shirika la Kimataifa la Helen Keller International Agosti 05, 2025 na kuzindua kambi maalum ya matibabu ya macho katika Kituo cha Afya Isimani, Wilaya ya Iringa.
Kambi hiyo ya siku saba inafanyika kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho na Helen Keller International, ikiwa ni juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya ya macho. Wananchi kati ya 600 hadi 700 wanatarajiwa kupata huduma za uchunguzi, ushauri wa kitaalamu, upasuaji wa macho pamoja na ufuatiliaji wa kiafya baada ya matibabu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mhe. Lukuvi alifikisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Helen Keller International na wadau wote waliowezesha kambi hiyo na kusema huduma zinazotolewa na shirika hilo zinaokoa maisha na kurejesha matumaini kwa wananchi.
Aidha Mhe. Lukuvi ameeleza kuwa Helen Keller International imekuwa mshirika wa karibu wa serikali kwa zaidi ya miaka 30, wakisaidia kuboresha afya na lishe nchini na kuwa kupitia ushirikiano huo, changamoto kubwa kama mtoto wa jicho na trachoma zimeendelea kupatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Iringa Mhe. Kheri James amewapokea wageni kutoka bodi ya shirika la Helen Keller International na kuwahakikishia kuwa serikali itawapa ushirikiano kuhakikisha wanafanya kile kinachotakiwa kuwasaidia wananchi na kuongeza kuwa Iringa ni salama hivyo wanakaribishwa.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa