Atoa wito kwa menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa pamoja na Baraza la Waheshimiwa Madiwani kujiimarisha kwenye suala la kubuni vyanzo vipya vya mapato kutokana na fursa ya kijiografia ya Halmashauri na mipaka yake.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Kheri James amesisitiza juu ya usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri kwani kuna mipango mingi ya kimaendeleo inayohitaji rasilimali fedha. Mhe. Kheri James amezungumza haya wakati wa mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani kwa robo ya pili uliofanyika Februari 28, 2025 katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo.
Aidha Mhe. James amehimiza Baraza na menejimenti kujiimarisha katika kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa kutumia fursa ya kimazingira na mipaka ya Halmashauri ikiwemo kuwekeza kwenye mazao ya kimkakati na skimu za umwagiliaji ili kuchechemua uchumi na kuongeza mapato na kwamba yeye mwenyewe na hata vyombo vyake vingine vitatoa ushirikiano pale utakapohitajika ili kuleta matokeo chanya.
“Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kijiografia imezungukwa na Halmashauri nyingi sana ambazo ni Manispaa ya Iringa, Mafinga, Mufindi, Kilolo, Mkoa wa Dodoma na Mbarali kwa upande wa Ruaha National Park ambayo ni fursa”, Amesema Mhe. James.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mhe. Steven Mhapa ametoa wito kwa waheshimiwa Madiwani Kwenda kusimamia miradi ya maendeleo iliyopo kwenye maeneo ya kata husika ili kujua mwenendo wa utekelezaji wake sanjari na kufanya kazi kwa ushirikiano kwa kuepuka majungu.
Mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani kwa robo ya pili 2024/2025 katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa pamoja na mambo mengine pia ulikuwa na jukumu la kujadili na kuthibitisha taarifa za kamati za kudumu za Halmashauri ambazo ni; Kamati ya Elimu, Afya na Maji, Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango, Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, Kamati ya Mapambano dhidi ya UKIMWI Pamoja na Kamati ya Maadili.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa