MKUU WA WILAYA YA IRINGA ATETA NA WATUMISHI WA IRINGA DC
Awaasa watumishi kufanya kazi kwa bidii na kuacha alama, ahimiza ubunifu kwenye utendaji hasa suala la vyanzo na ukusanyaji wa mapato
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Benjamin Sitta amefanya ziara kwenye ofisi za makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa – Ihemi ikiwa na lengo la kujitambulisha na kuongea na watumishi Agosti 12, 2025.
Mhe. Sitta ameambatana na wajumbe wa kamati ya usalama ya Wilaya Pamoja na maafisa Tarafa ambapo walitumia fursa hiyo kueleza masuala muhimu kwa watumishi.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Sitta amewaasa watumishi wa halmashauri kufanya kazi kwa bidii na kuwa wabunifu kwani kazi wanazozifanya zitawatambulisha.
“Mimi nawasisitiza kuweni wabunifu ukikaa na CMT yako umizini vichwa sana ni namna gani mnaweza kubuni vyanzo vipya ambavyo mkiwa na mapato mnaweza kujitanua zaidi, huduma itaongezeka zaidi lakini pia hata watu mambo madogomadogo mtaweza kuyatatua”
Aidha Mhe. Sitta amehimiza watoaji wa haki kuhakikisha kuwa wanasimamia hilo kwani imekuwa ni changamoto kubwa sana hasa kwenye masuala ya ardhi na kwamba viongozi wanapaswa kujipanga kuhakikisha kuwa kero mbalimbali za wananchi zinatatuliwa badala ya kuwasubiria viongozi.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ndugu Urassa amewahimiza watumishi wa Halmashauri ya Wilaya kuendana na mifumo iliyopo kwani kwa sasa vitu vingi vinategemea mifumo na kutoa wito kwa watumishi kuhakikisha kuwa wanazingatia ujazaji wa taarifa ya utendaji kazi (PEPMIS) kwani kutofanya hivyo kunaweza kupelekea usumbufu kwa mtumishi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ameeleza juhudi mbalimbali zinazofanywa na Halmashauri sanjari na changamoto zilizopo ikiwemo makazi na madai mbalimbali ya watumishi.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa