Wakumbushwa kutambua na kuthamini dhamana waliopewa na wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Kheri James akutana na wenyeviti wa vijiji wa Halmashauri ya Iringa na kuongea nao kuhusu uelekeo wa kiutendaji baada ya uchaguzi katika kikao kilichofanyika Januari 08, 2025 katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya iliyopo Mawelewele, Iringa mjini.
“Lazima tuwakumbushe kuwa ninyi ndio wenyeviti kwa kipindi cha miaka mitano hivyo lazima mjue kwa nini mlichaguliwa. Ukweli ni kwamba mmechaguliwa kwa sababu wananchi wenzetu wamewaamini hiyo ndio hoja ya msingi” amesema Mhe. Kheri.
Mhe. Kheri amewakumbusha viongozi kujipambanua kuwa ni viongozi wa mfano na ni viongozi ambao wanaweza kuaminiwa na watu waliowapa dhamana, hivyo kuwa mstari wa mbele katika mambo yanayopaswa kuwa katika Jamii kama kuwa kisima cha hekima, busara, haki, usawa, chachu ya maendeleo na hamasa ya umoja na mshikamano katika vijiji vyao.
Aidha Mhe. Kheri amewahimiza wenyeviti kijikita katika masuala makubwa ya msingi ambayo tayari Wilaya imejipambanua nayo ambayo ni; haki, usawa, maendeleo, umoja na mshikamano mambo ambayo yatatokea endapo kiongozi atakuwa Mwaminifu na mwenye kuaminika, mwadilifu, mbunifu, mwajibikaji na mwenye kuwasikiloiza wananchi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa amewapongeza wenyeviti wote wa vijiji 134 kwa kuchaguliwa na kuapishwa na kuwakumbusha kutambua kuwa wao sasa ni viongozi wa serikali za vijiji ambazo zina wajumbe wake na katibu wake ambaye ni Mtendaji wa Kijiji anayefanya kazi kama Mkurugenzi ngazi ya Kijiji.
Kwa upande wao wenyeviti wa vijiji kwa uwakilishi wametoa pongezi na shukrani kwa Mkuu wa Wilaya kwa kuandaa mafunzo haya ambayo yamewafungua ufahamu kwa sehemu kubwa na kuona kwamba hawapo peke yao bali kuna viongozi nyuma yao na kwamba wanaenda kufanyia kazi waliyoyapata ili kutoa matokeo Chanya.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa