Naibu Waziri Silinde Atoa Maelekezo Nane Uboreshwaji Elimu Msingi na Sekondari
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. David Silinde ametoa maagizo nane kwa Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi, Maafisa Elimu Msingi na Sekondari, Waratibu Elimu Kata pamoja na Wakuu wa Shule.
Maagizo hayo ameyatoa mapema leo katika kikao kazi cha mapitio ya tathmini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usimamizi wa elimu kwa mwaka 2022 na mpango wa mwaka 2023, kikao kilichofanyika katika ukumbi wa kichangani uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi kushirikiana kuhakikisha kuwa walimu wanatambuliwa hadhi zao na kutokudharauliwa na mtu yoyote. Pia amewataka Wazazi watambue umuhimu na kazi kubwa inayofanywa na waalimu.
“wanafunzi pia ni lazima wapate umahiri wa kusoma, kuandika na kuhesabu”, Kila kiongozi wa Elimu ahakikishe kuwa anafuatilia ufundishaji wa Waalimu darasani na kila mwalimu ajiwekee malengo binafsi katika masomo anayofundisha ili wanafunzi wote wapate umahiri. Amesema.
Amewataka viongozi wote kuhakikisha wanakomesha utoro kwa ngazi zote na ameagiza wazazi wahamasishwe uwepo wa chakula cha watoto mashuleni. Kadhalika ametaka pia kuwepo kwa kipimo cha utendaji na uwajibikaji wa kazi.
Aidha amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanahamasisha uandikishaji wa watoto darasa la Awali na Msingi na mwisho kabisa ameagiza Viongozi wote wawe wanafanya tathmini ya uwajibikaji wa watumishi.
Naye Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya Elimu Dkt. Charles Msonde amesema Serikali imegharamia fedha nyingi kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za elimu ikiwemo vitendea kazi kwa Maafisa Elimu ikiwa ni kurahisisha utendaji kazi.
Dkt. Msonde pia ameipongeza Serikali ya Mkoa wa Iringa kuwa miongoni mwa Mikoa michache inayofanya vizuri katika sekta ya elimu, aidha ameainisha changamoto mbalimbali zinazoonekana ni sababu za kutokufanya vizuri.
“kwa upande wa Shule za Msingi wanafunzi wengi bado hawajui kusoama na kuandika, lugha ya kiingereza pia bado ni changamoto, watoto wengi wanatoka darasa la saba hawajui kiingereza lakini changamoto nyingine ni utoro, kutokuwepo kwa chakula cha mchana na ufuatiliaji finyu wa maendeleo ya watoto” ameainisha.
Akitoa salamu za MKoa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa mhe. Halima Dendego amemshukuru Mhe. Rais kwa kuupatia Mkoa wa Iringa fedha za kutosha kwa ajili ya miradi na uendeshaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Aidha amesema miongoni mwa sababu za kutokufanya vizuri katika sekta ya elimu ni uhaba wa waalimu na amesema hakuna miujiza ya watoto kufaulu vizuri kama watoto hawatafundishwa hivyo ameitaka Serikali kulizingatia hilo.
“kama Mkoa umefanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuendelea kutatua changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo kwa wanafunzi na nyumba za walimu”. Ameongeza.
Kikao hicho kilicholenga kuja na maazimio ya pamoja kuhusu mapitio ya tathmini ya utekelezaji wa mikakati ya uboreshaji Elimu Msingi na Sekondari mwaka 2022 na mpango wa mwaka 2023 kimewakutanisha Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe. David Silinde, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa Dkt. Leonard Masanja, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wote wa Mkoa wa Iringa, Maafisa Elimu Msingi na Sekondari Wilaya na Kata pamoja na Wakuu wa Shule.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa