NGO’s zaaswa Kufanya Kazi kwa Kuzingatia Tamaduni za Kitanzania
“Serikali inasisitiza kuwa, Mashirika yasiyo ya Kiserikali yajitegemee zaidi kuliko kutegemea msaada kutoka nje ya nchi. Hii itasaidia kujijenga kiuchumi na kuendelea kudumu katika utoaji wa huduma na kufikia malengo, kwani misaada mingi ina masharti ambayo yanakiuka mila na desturi za Kitanzania”.
Kauli hii imetolewa na Kaimu Mkuu wa Wilaya Ndugu John Kiteve, ambaye ni mwakilishi wa Baraza la Taifa kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali – National Council of Non-Government Organizations (NACONGO), katika hotuba yake fupi kwenye kikao cha Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kilichofanyika Juni 02, 2023, kilichoandaliwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Aidha, Ndugu Kiteve ameendelea kusema kuwa, Serikali haitaruhu kupokea fedha kutoka kwenye Mashirika ambayo hayatazingatia tamaduni za Kitanzania, hivyo tuwe makini na misaada na fedha zao.
Ndugu Kiteve ameendelea kusema kuwa, “mikutano hii ni muhima sana kwani Serikali inatambua mchango wa Mashirika Binafsi na kuomba kuendelea kutoa ushirikiano ili kuimarisha dhana ya uwajibikaji na uwazi. Pia Mashirika yaelekezwe kujisajili kisheria pia kufanya kazi kwenye maeneo yenye uhitaji Zaidi huko vijijini”.
Katika kikao hicho pia Jukwaa limeweza kutoa taarifa ya Robo ya Kwanza ya Januari – Machi kwa kila shirika ambapo katika taarifa hizo zimeonesha utekelezaji wa shughuli zilizopangwa kufanyika kwa Robo hiyo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri Bi. Saumu Kweka amewashukuru Mashirika kwa muitikio wao katika kikao hicho, na kuwaomba kushiriki katika maandalizi ya sherehe za Siku ya Mtoto wa Afrika ambapo inategemewa kufanyika tarehe 15/06/2023 kwa Halmashauri, ambapo Sherehe hizo zitafanyika katika Kata ya Nzihi Kijiji cha Kidamali, na kwamba zimebebwa na Kauli Mbiu isemayo; “Zingatia Usalama wa Mtoto Katika Ulimwengu wa Kidigitali”.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa