RC Dendego Awaagiza Meneja wa TANROADS na TARURA Kuongeza Usimamizi na Ufuatiliaji kwa Wakandarasi
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego amewataka Meneja wa TANROADS na TARURA kuongeza usimamizi kwa wakandarasi wanaopewa kazi za matengenezo au ukarabati wa barabara.
Amesema wakati mwingine wakandarasi wanapewa kazi lakini hawana uwezo wa kutosha na kusababisha kero kwa wananchi na hasara kwa Serikali, kutokana na kutokukamilika kwa wakati au kujengwa chini ya kiwango kwa mujibu wa mikataba.
Ameyasema hayo mapema leo January 10, 2022 alipokuwa katika kikao cha Bodi ya barabara Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa (Siasa ni Kilimo).
Aidha amewaagiza Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Iringa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika miradi yote ya barabara na kutoa taarifa katika mamlaka zinazohusika wanapobaini kuwepo kwa dosari au kukiukwa kwa taratibu wakati wa matengenezo au ukarabati wa barabara.
"Ninamuagiza, Katibu Tawala Mkoa kuhakikisha kuwa sehemu ya miundombinu katika Sekretarieti ya Mkoa kutimiza wajibu wake kikamilifu wa kusimamia matengenezo na ukarabati unaofanywa na TARURA kwa sababu OR-TAMISEMI inatoa fedha za ufuatiliaji kwa kila robo mwaka". Ameagiza.
Kadhalika RC Dendego ametoa wito kwa wananchi kuacha kuvamia maeneo ya hifadhi ya barabara, kuswaga mifugo barabarani, kutupa taka kwenye mifereji ya barabara, na kuharibu alama za barabarani.
"Katika kipindi hiki cha mvua upo uharibifu mkubwa wa barabara unaofanyika kutokana na kuziba kwa nifereji inayopitisha maji kunakosababishwa na shughuli za kibinadamu, hali hii haipaswi kuendelea hatua zichukuliwe kwa wote wanaofanya uhujumu au uharibifu katika barabara".
Katika kikao hicho taarifa mbalimbali zimewasilishwa kutoka TANROADS na TARURA kuhusu utekelezaji wa matengenezo na ukarabati wa barabara kwa Mwaka wa Fesha 2020/2021 na 2021/2022 hadi Desemba 2022.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa