"TASAF Imetuheshimisha"- Walengwa wa TASAF IDC
Na Anthony Ramadhani,
Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bibi Agatha Lugome, wameongozana na Maafisa Habari wa Halmashauri kuwatembelea baadhi ya Walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya Maskini (TASAF) waliofanya vzuri katika kuboresha makazi, pamoja na miradi mbalimbali, kupitia fedha wanazozipata kutoka TASAF.
Walengwa hao wameonekana kufanya vizuri zaidi katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo kusomesha wanafunzi jambo ambalo hapo awali ilikuwa ni changamoto, baadhi yao pia wamejenga na kuboresha makazi yao pamoja na kuanzisha Miradi mbalimbali ya Kimaendeleo.
Wakizungumza katika mazingira tofauti tofauti walengwa hao wamewapongeza sana TASAF kwa uamuzi huo wa kuwasaidia na kuwakwamua kutoka kwenye umaskini na kuelezea namna ya walivyonufaika na mradi huo.
Leotina Mkisi mkazi wa Kijiji cha Iguluba Kata ya Malengamakali anasema Mbinu aliyoitumia katika kufikia mafanikio hayo ni kufanya uwekezaji mdogo mdogo alianza na kuku hadi sasa anamiliki ng'ombe na punda.
"Kwa kawaida watu huona fedha hizi ni ndogo na ni kweli ni ndogo lakini ukiamua kuzifanyia jambo la maendeleo haziwezi kuwa ndogo tena, mimi nilianza na uwekezaji mdogo tu, nilianza na ufugaji wa kuku baada ya muda kuku wangu wakazaliana na kuwa wengi kisha nikauza na kubakiza wachache ambao waliendelea kuzaliana pia".
Anaendelea kusema kuwa faida ile ya kuku akaamua kununua mbuzi na kwa muda wote huo akiwa anaendelea na ufugaji wa kuku, baadae tena baada ya mbuzi kuzaliana akaamua kuuza na kubakiza wachache kisha ile fedha akaitumia kununulia ng'ombe na punda na kwa sasa nina kuku, mbuzi, ng'ombe pamoja na Punda mmoja.
"Hivyo bila ya kufanya hivyo ni ngumu kuweza kutambua kuwa kuna uwezekanao mkubwa wa kufanya maendeleo makubwa kama haya, licha ya hayo pia nilikuwa na utaratibu wa kutunza fedha kidogo kwa njia ya Vikoba ambapo tulikuwa tunahifadhi fedha kule na mwisho wa siku tukawa tunagawana, nilikuwa sina hata vyombo ila kwa sasa nina vyombo vya kutosha, nimenunua nguo pamoja na kukarabati nyumba yangu.
Aidha amesema kuwa ana Mipango mingi anatarajia kufanya ikiwemo kuongeza mifugo na kuendelea kusomesha watoto wake.Mary Msigwa ni Mnufaika wa Mpango wa TASAF kutoka Kijiji cha Matembo Kata ya Kising'a anasema amekuwa akinufaika na mradi huu tangu mwaka 2015 na kwa kipindi chote hicho amekuwa akifanya maendeleo mbalimbali katika kaya yake ikiwemo ujengaji wa makazi, kuanzisha mifugo pamoja na shughuli za kilimo.
"Kwa upande wangu ninaishukuru sana TASAF imenisaidia fedha lakini si tu fedha bali hata elimu ya kutumia fedha hiyo, tulipatiwa elimu ya kujiunga na vikundi kama vile vikoba ambapo kule tuna utaratibu wa kukopeshana na kuhifadhi fedha na nimeweza kujenga nyumba ya vyumba vinne, nimesomesha na pia shughuli za kilimo imenisaidia sana kununua mbolea".
Monicka Samson Pamagila ni Mnufaika kutoka Kijiji cha Kihanga Kata ya Kihanga, Anasema kuwa maisha kabla ya TASAF yalikuwa ni magumu sana kwa upande wake ilifika wakati hata chakula kikawa ni shida kwake lakini mara baada ya mradi wa huu kuingia na kuchaguliwa na wanakijiji kuwa miongoni mwa wanufaika, maisha yake yameweza kubadilika kwa kiasi kikubwa.
"Mwanzoni nilikuwa na hali mbaya nilizoea kula mlo mmoja au kutokula kabisa lakini kwa hivi sasa tangu mradi hii uingie napata chakula vizuri, nakula mara tatu kwa siku navaa na sina shida ya chakula".
Kuhusu mbinu aliyoitumia yeye anasema kuwa alipokuwa anapata fedha hizi amekuwa na utaratibu wa kununua na kutunza mifugo ya nyumbani kana vile kuku, amekuwa akifanya hivyo kwa muda wote na huuza baadhi wanapokuwa wengi kisha fedha hiyo amekuwa akiitumia kwenye masuala ya chakula, mavazi pamoja na maradhi.
"Hata hii nyumba nayo nimeijenga kupitia fesda hizi hizi za Mradi hivyo mimi ninashukuru sana kuwepo kwa mradi huu, umenisaidia kutoka katika hali mbaya na sasa ninaishi kama watu wengine".
Katika halmashauri ya wilaya ya Iringa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unatekelezwa katika jumla ya vijiji 134 katika kata zote 28 zilizopo, na jumla ya kaya 10,351 mpaka sasa ndizo zinazoendelea kunufaika na ruzuku kupitia Mpango huu.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa