Utoaji Chakula Shuleni kwa asilimia 100 – DAS Michael
Kikao cha kujadili utekelezaji wa viashiria vya mkataba wa Lishe kimefanyika tarehe 21.7.2023.
Katika kikao hicho DAS amesisitiza utoaji wa chakula kwa shule zote kwa asilimia 100 na wanafunzi wote wapate chakula lengo ikiwa ni kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao pia kupambana na athari za lishe duni ikiwemo udumavu.
Aidha amewaagiza waratibu elimu na watendaji wa kata kusimamia suala hili kwa nguvu na liwe endelevu. "Waratibu elimu na watendaji Kata simamieni utekelezaji wa programu ya utoaji chakula kwa shule zote na wanafunzi wote wa kutwa na bweni wapate chakula cha mchana. Na si chakula pekee bali chenye uwiano sahihi wa virutubishi, hivyo kwa kutumia club za lishe anzisheni mashamba darasa, bustani za mbogamboga na matunda katika shule. Shirikianeni na maafisa ugani wa kilimo kuhimiza shule kulima chakula chenye viini lishe kwa wingi.
Kwa upande wake Afisa Lishe ametoa tathmini ya upimaji wa hali ya lishe kwa wanafunzi iliyofanyika katika robo hii imebaini uwepo wa wanafunzi wengi wenye ukondefu na miongoni mwao ni wale wasiopata chakula cha mchana wawapo shuleni, akiwasisitizia watendaji kushiriki katika vikao vya kamati za shule, bodi za shule na vikao vya wazazi kutoa elimu ya umuhimu wa utoaji chakula kwa wanafunzi.
Ameeleza zaidi kuwa katika umri balehe miaka 10-19 kunahitajika kula chakula kiasi cha kutosha kulingana na mahitaji ya mwili. Hivyo chakula chenye mchanganyiko kutoka katika makundi mbalimbali ya chakula ni muhimu sana katika umri huo ili kuwawezesha kuwa na lishe bora na imara kimasomo.
Ameeleza pia uhifadhi bora wa chumvi ngazi ya kaya ili kulinda madini joto yaliyomo ambayo ni muhimu sana kwa makundi lengwa (kaya zenye watoto chini ya miaka mitano na wajawazito). Kupitia sampuli zilizopimwa shuleni kutoka kutoka katika kaya zinaonyesha uwepo wa madini joto na chache hazina na ufuatiliaji umefanyika, hivyo elimu ya uhifadhi wa chumvi katika chombo chenye mfuniko, pasipo joto na unyevu ni muhimu sana kuzuia upotevu ambao unaweza kupelekea athari za kuvimba kwa tezi la shingo na uwezo mdogo wa ubongo kufanya kazi na pia wa darasani (ufaulu hafifu).
Kwa upande wa Watendaji wa kata za Migoli na Magulilwa wameomba mamlaka zinazosimamia sheria kuwachukulia hatua wazazi wanaokaidi kutekeleza uchangiaji wa programu ya utoaji chakula kwa wanafunzi.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa