Wafanyabiasha Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakutanishwa
Mwenyekiti wa TCCIA awakutanisha Wafanyabiasha wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Agosti 06, 2024, kwa lengo la kuunda Baraza la Wilaya ambalo litawasaidia katika mambo mbalimbali.
Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa TCCIA Ndugu Edmund Mkwawa amesema, “lengo la kukutana katika kikao hiki kwanza tufahamiane, pia kuunda Baraza ambalo litasaidia katika kutatua changamoto, kusaidiana kiuchumi na namna mbalimbali ya kutafuta masoko, pia kuisaidia Serikali”.
Aidha Mkwawa amesema, kuna faida nyingi katika umoja huo ambazo Mfanyabiashara atanufaika, kama namna bora kufungua kampuni, kujua vigezo na mipango vya namna ya kufanya biashara, kulinda sheria na kusaidiana kisheria.
Amesema, “kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa haijawahi kuwa na baraza la Wafanyabiashara na kupelekea watu kufanya mambo bila utaratibu au bila kujua nini kifanyike ili kutimiza malengo. Kwa kikao hiki tutachagua viongozi ambao watakuwa wanatuwasilisha katika mambo mbalimbali” amesema Mkwawa.
Naye Dr. Isdory Minani Mjumbe katika Baraza la Wafanyabiashara Mkoa na Mkuu wa Kitivo cha Biashara katika Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha amesema, “Lengo cha Chemba ni kuwaweka wafanyabiashara pamoja na kuwa sauti moja. Pia maoni ya wafanyabiashara yanachukuliwa na kutengeza Sera kwa kuisaidia Serikali”.
Ameongeza kusema kuwa, “tumezoea kufanya biashara kienyeji sana, sasa hivi mazingira, wateja na namna ya uendeshaji biashara yamebadilika, hivyo tujifunze teknolojia ya kisasa kufanya biashara, na nidhamu ya fedha lazima iwepo”.
Naye Afisa Biashara wa Halmashauri Ndugu Riziki Mhwagila amewaomba wafanyabiashara hao kuhudhuria vikao pindi watakapoitwa kwa lengo la kujadili mambo ya biashara. Hata hivyo uchaguzi wa viongozi haukufanyika kutokana na waliohudhuria kutotimia akidi.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa