“Waliosabaisha Hoja Wachukuliwe Hatua” – RC Dendego
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mheshimiwa Halima Dendego alipokuwa akifungua Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani tarehe 13/06/2023 ambao ulikuwa unajadili hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, zilizopatikana kwa mwaka wa Fedha unaoishia Juni 30, 2021/2022.
Mheshimiwa Dendego amesema, “Kila Halmashauri ina wajibu wa kujibu hoja ambazo zimepatikana katika mwaka husika, hivyo ni muhimu kuwajua waliosababisha hoja na kuwachukulia hatua bila kuwafumbia macho.”
Aidha, Mheshimiwa Dendego amewasihi Madiwani wa Halmashauri hiyo kusimamia miradi ya maendeleo na ukusanyaji wa mapato, na kila Robo ya mwaka wakae na kufanya tathmini kuwa imekusanywa kiasi gani. Pia amewataka Madiwani hao kufanya vikao vya Kata na kwamba mapato iwe agenda ya kudumu.
Kadhalika Mheshimiwa Dendego ameiasa Menejimenti ya Halmashauri kuwa, inapaswa ikutane kila mwezi na agenda ya hoja iwe ya kudumu, na kwamba waliosababisha hoja wajulikane.
Pamoja na mambo mengine Mheshimiwa Dendego amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri Wakili Bashir P. Muhoja kwa kuendelea kuaminiwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuendelea kuongoza Halmashauri. Pia ameipongeza Halmashauri kwa kupata Hati Safi kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022, na kuipa heshima Mkoa wa Iringa. Jambo hili limetokana na ushirikiano wa viongozi wote na watumishi.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa Ndugu Leonard Masanja amesema, maoni yaliyopendekezwa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ni hatua za kisheria, hivyo ni muhimu kuzifanyia kazi na hoja zote ziondolewe.
Ameongeza kusema kuwa, “nawaomba Madiwani kuhamasisha wananchi kulipa kodi, kusimamia matumizi ya Halmashauri pia kufanya kazi na Mkaguzi wa Ndani ni muhimu ili kupunguza hoja”.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kukubali kuja kwenye Mkutano huo, na kuahidi yale yote yaliyosemwa pamoja na Madiwani wake wataenda kuyafanyika kazi ili kuijenga Halmashauri.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa