Watendaji wa Kata, Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule Wajiandaa Vema Kupokea Wanafunzi Kidato cha Kwanza 2023
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja amewapongeza Watendaji wa Kata, Maafisa Elimu Kata na Wakuu wa Shule kwa kufanya kazi nzuri ya kusimamia vema ujenzi wa vyumba vya madarasa yanayotarajiwa kupokea wanafunzi wa Kidato cha Kwanza 2023.
Wakili Muhoja ametoa pongezi hizo alipokutana na Watendaji hao ili kujua mafanikio na changamoto katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, ambavyo kwa sasa ujenzi huo unaelekea mwishoni tayari kwa kupokea wanafunzi.
“Nawapongeza sana kwa kazi zinazofanyika kwa kipindi chote ambacho ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa baadhi ya shule ulikuwa unaendelea. Tuendelee kusimamia vema hadi pale wanafunzi wa Kidato cha Kwanza watakapokuwa wanaingia katika vyumba vya madarasa vikiwa safi na kila chumba kuna viti na meza kwa idadi sawa na wanafunzi waliopangwa”.
Pamoja na mafaanikio hayo Watendaji hao walieleza baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na upungufu wa viti na meza kwa baadhi ya shule, wananchi kutochangia miradi ya maendeleo ambapo inasababisha miradi kutokamilika kwa wakati.
Wakili Muhoja akifafanua changamoto hizo amesema, “Pamoja na changamoto hizi lakini tujitahidi kukamilisha ujenzi kabla shule hazijafungua, elimu itolewe kwa wananchi juu ya uchangiaji maendeleo na kwamba kwa kushirikiana wote pamoja tutafikia lengo”,
Halmashauri ya Wilaya ya Iringa inatarajia kupokea wanafunzi wa Kidato cha Kwanza 7929 kwa mwaka 2023.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa