Watoto Waomba Wazazi/Walezi Kusikilizwa Shida Zao
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika hufanyika kila ifikapo Juni 16 Barani Afrika na Tanzania nzima. Kwa upande wa Halmashauri ya Wiaya ya Iringa Maadhimisho hayo yamefanyika Juni 15, 2023 katika Kata ya Nzihi Kijiji cha Kidamali, ili kuweza kusherehekea Kimkoa ifikapo 16 Juni.
Katika Maadhimisho hayo Watoto wameweza kupaza sauti zao na kuwaomba wazazi/walezi kuwasikiliza pale wanapokuwa na shida pia kushirikishwa katika maamuzi ambapo ujumbe wao walitoa kwa njia ya Risala, nyimbo na burudani mbalimbali.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Stephen Mhapa ambaye alikuwa Mgeni Rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya amesema kuwa, “sherehe ya leo imenifundisha mambo mengi sana hasa kwenye Risala, ambayo imeongea mambo mengi. Japo hotuba hii ni Mkuu wa Wilaya lakini mimi nimesoma kwa niaba yake. Nawapongeza Watoto kwa kuwasilisha hisia zao na kwamba sisi wazazi/walezi tuna wajibu wa kuyafanyika kazi”.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji (Huduma za Jamii) Mheshimiwa Felix Waya amesema, “ili malezi ya mtoto yaweze kukamilika anatakiwa kupatiwa chakula kuanzia akiwa na umri wa mwaka sifuri. Baraza la Madiwani limeweka maazimio kuwa, ifikapo Julai, shule zote ziwe zinachangia chakula ili Watoto wapate lishe na afya katika masomo yao.Hii inatokana na hali ya udumavu iliyopo katika jamii yetu”.
Aidha, Mheshimiwa Waya amewashukuru Wadau kwa kujitoa katika elimu na kuhudumia jamii katika maeneo mbalimbali.
Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bi. Saumu Kweka ambaye amemuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, amewashukuru Wadau kwa michango yao ya hali na mali katika kuhakikisha jamii inakuwa salama.
Kwa upande wake Mkaguzi wa Dawati la Jinsia na Watot la Polisi Iringa Inspekta Lidia Sospeter amesema, simu ni chanzo cha ugomvi kati ya baba na mama hadi kupelekea familia kutengana na kusababisha Watoto kuhangaika. Pia wazazi wajitahidi kufuatilia vipindi vya Runinga ambavyo Watoto huwa wanaangalia ili kujua kama wanaangalia vipindi vya aina gani.
Ameendelea kusema kuwa, wazazi wawe na tabia ya kuwakagua Watoto hasa wakati wa kuoga ili kugundua madhira wanayopata. Vilevile wazazi/walezi wawafuatilie Watoto wasipende michezo ya kamari ambayo itawaingiza katika vishawishi.
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yam waka 2023 yamebebwa na Kauli Mbiu isemayo; “Zingatia Usalama wa Mtoto Katika Ulimwengu wa Kidigitali”.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa