WATUMISHI WA AFYA WAASWA KUZINGATIA MAADILI YA KAZI
Watumishi wa afya waaswa kuzingatia maadili ya kazi na kutofanya kazi kinyume na walichofundishwa pamoja na viapo walivyokula. Haya yamesemwa na Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe alipokuwa akizungumza na viongozi pamoja na wataalamu mbalimbali wa afya Mkoani Iringa tarehe 16/07/2023 katika Ukumbi wa Siasa ni Kilimo.
“Kila mtu alikula kiapo kwa kadri ya taaluma yake tuzingatie, siri, utoaji wa huduma kwa viwango, weledi na suala zima la ufanisi” amesema Dkt. Magembe. Aidha suala la usalama katika eneo la kazi kwa watumishi wa afya limesisitizwa na kwamba vifaa vya kujikinga vitumiwe kikamilifu.
Naye Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Dkt. Wilson Mahera amesema kuwa suala la uhamisho kwa watumishi linafanyiwa kazi na kwamba watumishi walioomba uhamisho wawe watulivu na waepuke matapeli.
Kwa upande wa elimu Dkt. Mahera amesema fedha nyingi sana zimetolewa kwenye miradi ya ujenzi wa madarasa ya Boost hivyo kasi ya ujezi iongezwe ili ujenzi uweze kukamilika kwa wakati na kwamba Wakurugenzi wachukue jukumu hili kuhakikisha kwenye mradi mafundi wanakuwa wengi.
Pia kwenye upande wa afya Dkt Mahera amesisitiza kuwa Serikali ipo mbioni kutoa magari mawili ya kubebea wagonjwa (Ambulance) kwa kila Halmashauri ili kuendelea kuboreha upatikanaji wa huduma.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha nyingi sana kwaajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwenye Idara ya afya ambapo mwaka huu tu zahanati 11 zinaenda kufunguliwa Halmashauri ya wilaya ya Iringa, Hospitali ya Wilaya imejengwa, Jengo la makao Makuu na Miradi mingine mingi ya Elimu inatekelezwa.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa