Mh. Ndejembi Aipongeza Iringa DC kwa Kutatua Kero za Watumishi
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mh. Deogratius John Ndejembi, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Utumishi kufanyia kazi madeni ya watumishi ndani ya Halmsashauri zao.
Mh.Ndejembi, amesema hayo wakati akiongea na watumishi wa Halmashauri mbili za Wilaya ya Iringa na Manispaa ya Iringa, kuwa Watumishi wa Umma wana haki ya kupandishwa madaraja ikiwa ni pamoja na kupewa stahiki zao za msingi.
“Muweke utaratibu wa kukaa na kusikiliza kero za watumishi wenu, kisha mzibebe changamoto zao na kuzifanyia kazi” alisema Mh. Ndejembi.
Aidha, Mh. Ndejembi, amewataka Viongozi wa Serikali kutoumizana kwenye mazingira ya kazi kwakuwa ufanisi wa kazi wa mtumishi ndio sifa ya Mkurugenzi au Mkuu wa Idara husika, ikiwa ni pamoja na kuwahudumia wananchi kwa moyo.
Sambamba na hayo, Mh. Ndejembi amewataka watumishi wote wa Umma kufanya kazi kwa mpangilio ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuandika taarifa ya kila kinachofanyika. (Progress Report).
Ameongeza kusema kuwa, kufanya mawasiliano kati ya mtu na mtu ndani ya Idara au Idara na Idara ili kuondoa mkanganyiko katika utendaji kazi.
Naye Mkuu wa Wilaya Mheshimiwa Mohamed Moyo alikuwa na haya ya kusema; “Tunashukuru kwa kutoa pesa kwa ajili ya ujenzi wa Halmashari ya Wilaya ya Iringa ambayo imejengwa katika Kata ya Mgama Kijiji cha Ihemi. Lakini kuna changamoto ya nyumba za watumishi, hivyo watumishi watatumia gharama kubwa sana katika usafiri, hivyo naomba zijengwe nyumba za watumishi ili wafanye kazi kwa ufanisi.”
Mh. Moyo ameongeza kusema kuwa, amejifunza mambo mengi ya Kiutumishi katika kikao hicho, na kwamba amewaomba watumishi kutosubiri Mawaziri waje ndipo watoe malalamiko yao, ili hali kuna Mkurugenzi ambaye ataweza kushughulika na malalamiko hayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashari ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja, ameipongeza Ofisi ya Utumishi Wilaya kwa kushughulikia vema matatizo ya Watumishi hadi kupelekea kupata tuzo kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022, na kwamba kwa sasa malalamiko ya watumishi yamepungua kwa kiasi kikubwa.
Wakili Muhoja ameiomba Serikali kuongeza bajeti kwa ajili ya mahitaji na stahiki za Wakuu wa Idara na aweze kuwalipa kwa wakati, kwani kwa wakati huu anashindwa kuwatimizia mahitaji yao yote kwa wakati mmoja kutokana na ufinyu wa bajeti.
Pia Wakili Muhoja ameomba kuongezewa ikama ya watumishi kwa Kada mbalimbali kwani kila Idara ina upungufu wa watumishi.
Ameongeza kwa kusema kuwa, mikopo inayotoka Serikali Kuu kwa ajili ya Watumishi haitoshelezi, kwani wahitaji ni wengi na kuomba kuongeza kiasi angalau kila muhitaji apate kulingana na maombi.
Wakili Muhoja amemaliza kwa kuomba vitendea kazi hasa kwa upande wa Watendaji wa Kata. Halmashauri imeweza kununua pikipiki 15 tu hivyo uhitaji bado ni mkubwa sana.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa