“Serikali Inatengeneza Mifumo Ili Kumrahisishia Mtumishi Katika Utendaji Kazi” – Mh. Kikwete
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – Utumishi Mheshimiwa Ridhiwan Kikwete amefanya ziara Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Nov 23, 2023 na kuweza kuongea na watumishi kwa kusikiliza kero zao.
“Serikali inaendelea kutengeneza mifumo wezeshi ili kumrahisishia mtumishi katika utendaji kazi wake, na kupata taarifa mbalimbali za kiutumishi, kama kukopa fedha benki, taarifa binafsi. Kupitia mifumo mtumishi anaweza kuomba uhamisho mahali popote alipo na kufanya maombi mengine mbalimbali”.
Mheshimiwa Kikwete ameendelea kusema, Ofisi ya Utumishi inawajibu wa kumkumbusha mtumishi juu ya wajibu wake mahala pa kazi na nje ya kazi, kufuata Kanuni za utumishi wa Umma na stahiki zake.
Aidha Mheshimiwa Kikwete amesema, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassana ameendelea kupandisha vyeo watumishi mbalimbali, kuwabadilishia watumishi miundo kwa zaidi ya watumishi 5,000, kutoa ajira mpya na ajira mbadala. Kwa mwaka huu wa fedha Serikali itatoa ajira zaidi 47,374, 000 kwa Watanzania, pia kuendelea kulipa malimbikizo ya mishahara na madeni mbalimbali yasiyo ya mishahara, kufanya uhamisho.
Pia Mheshimiwa Kikwete amemuagiza Mkurugenzi kuandika barua na kuwasilisha madeni yote yanayodaiwa na Watumishi wake.
Mheshimiwa Kikwete ametoa ombi kwa watumishi kuwa, waendelee kufanya kazi ili tija ya kiutumishi ionekane, kudumisha viapo vya maadili ya kazi na kuacha kufanya kazi kimazoea.
Pia ametoa maagizo kwa kusema, Mamlaka ziendelee kusimamia nidhamu, kuweka malengo bayana ya kiutendaji, na wajibu wa kila mtumishi kuwajibika katika eneo lake.
Mheshimiwa Kikwete amemshukuru Rais kwa kumuamini na kumpa kuwa msaidizi katika Wizara hii. Pia amempongeza Mkurugenzi kwa kusimamia miradi na kuongoza vizuri Halmashauri.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Stephen Mhapa ameishukuru Serikali kwa kuleta miradi mingi katika Halmashauri, na kuomba kuongeza kwa watumishi katika vituo ambavyo kuna uhaba wa watumishi kama zahanati na shule. Pia uhaba wa Watendaji wa Kata na vijiji ambapo inakuwa tatizo katika kusimamia miradi na hasa ikizingatiwa mwaka ujao kutakuwa na chaguzi mbalimbali za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwe Mhapa ameongeza kusema juu ya kikokotoo cha wastaafu ni tatizo, kwani wengi wanapoteza maisha kwa mawazo ya kikokotoo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Wakili Bashir Muhoja amemshukuru Mheshimiwa Kikwete kwa kuja kutembelea Halmashauri pia kuongea na watumishi. Na changamoto zote zilizotolewa amezichukua na kwenda kuzifanyia kazi.
Kadhalika Watumishi hao waliweza kutoa kero zao mbalimbali na Mheshimiwa Kikwete amezijibu na kuziwasilisha sehemu husika kwa hatua zaidi.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa